Baraza la Usalama laitisha kikao kujadili hali ya Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i120990-baraza_la_usalama_laitisha_kikao_kujadili_hali_ya_gaza
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitisha kikao ambacho ajenda yake kuu ni kuchunguza mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-01-04T03:50:11+00:00 )
Jan 04, 2025 03:50 UTC
  • Ammar bin Jame
    Ammar bin Jame

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitisha kikao ambacho ajenda yake kuu ni kuchunguza mashambulizi ya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Ammar bin Jame, Mwakilishi wa Algeria katika kikao hicho ameeleza kuwa lengo la mashambulizi na mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya watu wa Gaza ni kuwafukuza Wapalestina katika ardhi yao kupitia sera za maangamizi ya kizazi. 

Bin Jame amesema asilimia 63 ya hospitali za Ukanda wa Gaza hazifanyi kazi na zaidi ya magari ya wagonjwa 100 yameharibiwa na kuongeza kuwa, Israel inazishambulia taasisi za tiba na wafanyakazi wa taasisi hizo. 

Mwakilishi wa Algeria ameeleza kuwa utawala wa Israel umeichoma moto kwa makusudi Hospitali ya Kamal Adwan huko kaskazini mwa Ukanda wa Gaza ili kuwazuia wakazi wa eneo hilo kupata matibabu. 

Hospitali ya Kamal Adwan iliyochomwa moto na Israel

"Kitendo cha Israel cha kuwakosesha matibabu wakazi wa Gaza na kuwalazimisha kuhama makazi yao kupitia kuzishambulia hospitali, ni jinai ya kivita", amesema Ammar bin Jame.  

Katika kikao hicho cha Baraza la Usalama la UN, Mwakilishi wa Russia pia amekosoa mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika maeneo ya raia na taasisi za huduma ya matibabu na kusema vitendo hivyo visivyo vya kibinadamu vinapasa kukomeshwa. 

Wakati huo huo Linda Thomas Greenfield Mwakilishi wa Marekani katika Baraza la Usalama ameunga mkono mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.