Kuendelea hatua za kimataifa dhidi ya uvamizi wa Israel
Katika kuendeleza mapambano na kupinga jinai za Israel dhidi ya Wapalestina, viongozi wa Afrika Kusini, Malaysia na Colombia wametangaza kuwa watazizuia meli zilizobeba silaha kwa ajili ya Israel kuingia katika bandari za nchi hizo.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, Anwar Ibrahim Waziri Mkuu wa Malaysia na Rais Gustavo Petro wa Colombia wameashiria katika makala yao ya pamoja kwenye jarida la Foreign Policy kwamba wanataka kuhitimishwa kinga inayoupa utawala wa Kizayuni haki ya kukika sheria za kimataifa na kutahadharisha kuwa: Chaguo liko wazi; ama kwa pamoja tuchukue hatua ili kutekeleza sheria za kimataifa, au tutakuwa katika hatari ya kuporomoka.
Viongozi wa nchi hizi tatu pia wamesema kuwa watazizuia meli zinazobeba silaha kwa ajili ya utawala wa Israel zinazoingia katika bandari za nchi hizo na kuongeza kuwa: Watazuia upelekeaji wowote wa silaha ambao unakiukwa sheria za kibinadamu.
Afrika Kusini, Malaysia na Colombia zimechukua uamuzi huu katika hali ambayo baadhi ya nchi duniani hasa, Marekani na Ujerumani, zinaendelea kutuma silaha na zana za kijeshi kwa Tel Aviv ikiwa ni muendelezo wa kuuhami utawala wa Kizayuni katika mauaji yake ya kimbari dhidi ya Wapalestina. Ben Saul Ripoti Maalumu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na haki za binadamu na mapambano dhidi ya ugaidi amesema kuhusua hili kwamba: Karibu asilimia 69 ya silaha na zana za kijeshi za Israel hutolewa na Marekani, na karibu asilimia 30 hutolewa na Ujerumani.

Katika mazingira kama haya, uamuzi wa Afrika Kusini, Malaysia na Colombia unaweza kuhesabiwa kuwa una mwelekeo tofauti wa kisiasa, haki za binadamu, kimataifa na kiuchumi.
Katika uga wa haki za binadamu na kimataifa, moja ya vipengele muhimu vya hatua hii ni jibu kwa sera na maamuzi ya upande mmoja ya Marekani na nchi za Magharibi ambazo siku zote zimekuwa zikiikingia kifua na kuihami Israel. Inaonekana kuwa aghalabu ya nchi za Afrika na Amerika ya Latini na Kusini mwa bara Asia zinataka kuweko mlingano wa nguvu na zinasisitiza udharura wa kuwajibika katika mfumo wa kimataifa. Kwa msingi huo, hatua ya Afrika Kusini, Malaysia na Colombia ya kutamka bayana kuwa zitazuia meli zinazobeba silaha kwa ajili ya Israel inalenga kuzuia machafuko zaidi na ukiukwaji mkubwa haki za binadamu.
Katika upande mwingine, hatua mpya ya pamoja ya Afrika Kusini, Malaysia na Colombia inaweza kutajwa kama jibu kwa sera za kiuchumi na kijeshi za madola makubwa hasa Marekani. Ni dhahir shahir kuwa nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, zinapata faida kubwa ya maelfu na mabilioni ya dola kwa kuiuzia silaha na zana zana za kijeshi Israel. Kwa msingi huo, hatua hiyo itawaongezea gharama na hatimaye itasababisha mashinikizo ya kiwango fulani kwa madola makubwa na kuyafanya yaangalie upya sera zao za silaha na uungaji mkono utawala wa Israel. Vilevile inaweza kuwa na taathira kwa minyororo ya kimataifa ya uuzaji silaha katika kuiunga mkono Israel. Ni jambo lililo wazi kwamba, kwa kuzingatia kuwa uchumi wa dunia kwa sasa umefungamana pakubwa na biashara ya silaha na uuzaji nje wa zana za kijeshi, harakati na upinzani kama hi huenda ukaibua changamoto kwa makampuni ya silaha na wauzaji wakuu wa silaha.
Pamoja na hayo, sera hizi zitakabiliwa na changamoto kubwa. Madola makubwa hususan Marekani, yanaweza kutumia wenzo kama vile vikwazo na vizuizi vya kibiashara kuziwekea nchi hizo mashinikizo ya kiuchumi na kisiasa. Hata hivyo, hatuua ya Afrika Kusini, Malaysia na Colombia ya kupiga marufuku meli zinazopeleka silaha kwa utawala wa Israel, licha ya kuwa ni hatua muhimu kwa jaili ya kulinda haki za binadamu na sheria za kimataifa, inaweza kuathiri pakubwa sera za kimataifa na mahusiano ya kiuchumi ya kimataifa. Nchi hizo zimeonyesha kuwa ziko tayari kukabiliana na sera za uvamizi na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Hatua kama hizi zilizochukuliwa na viongozi wa Afrika Kusini, Malaysia na Colombia na kutangaza wazi kwamba watazuia meli zinazobeba silaha kwa ajili ya Israel kuingia katika bandari zao, ingawa hazizuii kutumwa silaha kwa utawala huo, lakini zinatuma ujumbe mzito kwa jamii ya kimataifa kuwa nchi nyingi haziko tayari tena kunyamaza kimya mkabala wa ukiukaji wa haki za binadamu na uvamizi wa kijeshi wa Israel.