Serbia: Tunakabiliwa na 'mapinduzi ya rangi' ya Magharibi
Naibu Waziri Mkuu wa Serbia, Aleksandar Vulin amesema nchi hiyo ya eneo la Balkan inawajihiwa na tishio la "mapinduzi ya rangi" kutoka nchi za Magharibi.
Vulin ameshutumu idara za usalama za nchi za Magharibi kwa kupanga machafuko ili kuchochea kupinduliwa kwa serikali ya nchi hiyo, sawa na 'Mapinduzi ya Maidan' ya Ukraine ya 2014.
Maandamano yanayoongozwa na wanafunzi kulalamikia madai ya ufisadi na uzembe wa serikali yamekuwa yakiendelea nchini Serbia kwa miezi kadhaa sasa.
Maandamano hayo yaliyoanza tangu Novemba 2024, yalipamba moto huko Belgrade mnamo Machi 15, na kupelekea kuibuka makabiliano makali kati ya makumi ya waandamanaji na askari polisi.
"Mapinduzi ya rangi yanafanyika Belgrade," Vulin alisema jana Jumamosi, wakati wa mkutano wake huko Moscow na Katibu wa Baraza la Usalama wa Taifa la Russia, Sergey Shoigu.
Ameeleza bayana kuwa, "Huduma za usalama za nchi za Magharibi ziko nyuma ya mapinduzi ya rangi, kwani zinataka kuweka serikali mpya madarakani," akiongeza kuwa mamlaka za Serbia "hazitaruhusu (hilo kufanyika)."
Rais wa Serbia, Aleksandar Vucic huko nyuma pia aliwashutumu 'maajinabi' kwa kuchochea machafuko ili kuyumbisha nchi hiyo, akidai kuwa vikosi vya upinzani vinashirikiana na mashirika ya kijasusi ya Magharibi, Croatia na Albania ili kuipindua serikali yake.