ASEAN kufanya mikutano kuhusu Myanmar
Jumuiya ya mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia, ASEAN inatarajia kuiitisha mikutano miwili mahsusi kwa ajili ya kkujadili hali ya mambo nchini Myanmar.
Ripoti zinasema kuwa, mikutano hiyo miwili ni maandalizi ya kuelekea mkutano wake wa kilele wiki ijayo.
Haya yamesemwa na katibu mkuu wa jumuiya hiyo Kao Kim Hourn.
Kim Hourn hakuweka wazi masuala yatakayojadiliwa kwenye mikutano hiyo au ikiwa kuna mapendekezo mapya yatakayotolewa.
Jumuiya hiyo ya ASEAN yenye idadi ya wanachama 10, imekuwa ukitoa wito wa kusitishwa mapigano kati ya waasi na wanajeshi wanaoitawala Myanmar, ambayo yamesababisha karibu watu milioni 3.5 kuachwa bila makazi, tangu jeshi lilipomuondoa madarakani rais aliyechaguliwa Aung San Suu Kyi mwaka 2021.
Jeshi la Myanmar lilitwaa madaraka ya nchi Februari Mosi mwaka 2021 baada ya kumkamata Rais wa nchi, Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi mkubwa, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo.
Kisingizio cha jeshi cha kufanya mapinduzi hayo ni madai yake ya kutokea wizi na udanganyifu katika uchaguzi wa Bunge wa Novemba mwaka jana ambapo chama tawala cha National League for Democracy (NLD) kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kiliibuka na ushindi.
Katika upande mwingine, Waislamu ni jamii ya wachache katika nchi ya Myanmar inayotawaliwa na Wabudha walio wengi, na wamekuwa wakikandamizwa na kutengwa na serikali, huku makundi ya kitaifa yenye misimamo mikali yakichochea vurugu katika miaka ya hivi karibuni. Waislamu wa Rohingya, kundi kubwa la wachache, ni miongoni mwa walioteswa sana na mamlaka za Myanmar, wakikumbwa na vifo vya halaiki na kufukuzwa.