Mfanyabiashara wa Kifaransa ajitolea kulipa faini za wanawake Waislamu wanaovaa Burkini
-
Rashid Nakaz
Rashid Nakaz, mfanyabiashara tajiri na mwanaharakati wa kisiasa wa Ufaransa ametangaza kuwa atalipa faini wanazotozwa wanawake Waislamu wanaovaa vazi la kuogelea linalojulikana kwa jina la Burkini.
Nakaz ametangaza msimamo huo kwa lengo la kupambana na sheria iliyopitishwa nchini Ufaransa ya kupiga marufuku uvaaji wa vazi hilo linalomsitiri mwanamke wakati anapoogelea.
Hadi sasa mfanyabiashara huyo ameshatumia pauni laki mbili kulipa faini za sheria zilizowekwa katika nchi za Ulaya dhidi ya wanawake wa Kiislamu wanaovaa nikabu.
Rashid Nakaz, tayari ameshalipa faini za wanawake watatu Waislamu ambao wamevaa vazi la Burkini licha ya kupitishwa sheria nchini Ufaransa ya kupiga marufuku uvaaji wake na ametangaza kuwa yuko tayari kulipa faini za wanawake wengine watakaochukua hatua ya kuvaa vazi hilo.
Burkini ni aina ya vazi la kuogelea kwa ajili ya wanawake wanaovaa hijabu, ambalo linamsitiri mwanamke mwili mzima isipokuwa uso na viganja vya mikono na miguu. Neno Burkini limetokana na muungano wa maneno mawili ya Burqa na Bikini.
Nakaz ametangaza kuwa yeye binafsi hakubaliani na uvaaji wa burkini na nikabu lakini anaitakidi kuwa katika mfumo wa kidemokrasia haifai kuwazuia watu kuchagua vazi binafsi la kuvaa kwa sababu vazi hilo "halihatarishi uhuru wa watu wengine au usalama wa nchi".
Mnamo mwaka 2010, na kufuatia kupigwa marufuku uvaaji wa nikabu katika nchi za Ufaransa na Ubelgiji, mfanyabiashara huyo tajiri alianzisha "Mfuko wa Kutetea Uhuru wa Binafsi" wa yuro milioni moja kwa madhumuni kuwalipia faini wanawake wanaoamua kuendelea kuvaa vazi la nikabu.
Nakaz ameliambia gazeti la Telegraph:"kila ninapoona nchi ya Ufaransa haiheshimu uhuru wa msingi nami huamua kutumia cheki yangu".../