UNICEF: Watoto milioni 50 wamekimbia makwao duniani
Karibu watoto milioni 50 duniani wamekimbia makazi yao, zaidi ya nusu ya idadi hiyo ikiwa ni kutokana na mizozo na mapigano kwenye nchi zao.
Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, katika ripoti yake iliyotolewa leo Jumatano ikiangazia ongezeko la janga la wakimbizi na wahamiaji watoto.
Ripoti hiyo imesema idadi iliyosalia wanakimbia makwao kusaka maisha bora na usalama lakini wakiwa njiani hukumbwa na majanga zaidi kukiwemo kuzama baharini, njaa, utapiamlo na hata usafirishaji haramu.
Mkurugenzi mkuu wa UNICEF Anthony Lake anahoji ni mustkabali gani ambao unaandaliwa iwapo watoto hao hawana uhakika wa maisha yao? Ili kukabiliana na hali hiyo anasema UNICEF imependekeza mambo sita kukiwemo kulindwa watoto wahamiaji na wakimbizi wanaosafiri wenyewe dhidi ya ghasia na ukatili, kuondoa uwekaji korokoroni watoto wanaosaka hifadhi na kuweka mbinu mbadala.
Hali kadhalika familia kuwekwa pamoja, watoto hao kupatiwa fursa ya kujifunza, kushughulikia masuala yanayoshinikiza watoto kukimbia na kuendeleza hatua za kukabiliana na chuki dhidi ya wageni na ubaguzi.
UNICEF inasema Uturuki ndiyo yenye idadi kubwa zaidi ya watoto wakimbizi na wahamiaji kulingana na idadi ya watu wake sanjari na Lebanon ambako mtu mmoja kati ya watano ni mkimbizi.