Sep 17, 2016 02:40 UTC
  • Shambulio la kigaidi msikitini laua makumi ya watu Pakistan

Watu wasiopungua 23 wameuawa na makumi ya wengine wamejeruhiwa katika shambulio la kigaidi lililofanywa ndani ya msikiti katika Sala ya Ijumaa wilayani Mohmand nchini Pakistan.

Duru za habari zimeripoti kuwa shambulio hilo la jana lilifanywa katika kijiji cha Anbar Tehsil kilichoko kwenye eneo la kikabila la kaskazini magharibi mwa Pakistan katika mpaka wa pamoja wa nchi hiyo na Afghanistan.

Naveed Akbar, Naibu Mkuu wa wilaya wa Mohmand amesema, mshambuliaji aliyejifunga mada za miripuko aliyekuwa ndani ya msikiti uliofurika waumini alipaza sauti juu kupiga takbir na mara mripuko mkubwa ukatokea.

Ameongeza kuwa idadi ya vifo imechangiwa pia na kuporomoka sehemu ya jengo la msikiti kutokana na nguvu ya mripuko huo na kuwaangukia watu waliokuwemo ndani yake. 

Japokuwa hakuna aliyetangaza kuhusika na shambulio hilo lakini kundi la kigaidi la Taliban ya Pakistan limekuwa likishambulia mara kwa mara maeneo yasiyo na ulinzi mkubwa ya eneo hilo kama majengo ya mahakama, shule na misikiti.

Hali msikitini baada ya kutokea mripuko

Mnamo mwezi Juni 2014, jeshi la Pakistan lilianzisha operesheni ya kuyatokomeza makundi yanayobeba silaha katika maeneo ya kikabila huko kaskazini magharibi mwa nchi kwa lengo la kuhitimisha wimbi la machafuko lililoanza mwaka 2004 na kusababisha vifo vya maelfu ya raia.

Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif amelaani shambulio hilo la jana na kueleza kuwa: "Mashambulio yanayofanywa na magaidi hayatovuruga azma ya serikali ya kuutokomeza ugaidi nchini".

Hali ya usalama imeboreka nchini Pakistan katika miaka ya karibuni, ambapo kwa mujibu wa jeshi, idadi ya "matukio ya kigaidi" imepungua kutoka 128 mwaka 2013 hadi 74 mwaka uliopita wa 2015, japokuwa mashambulio makubwa katika maeneo yaliyo rahisi kushambuliwa yangali yanaendelea kushuhudiwa.../

Tags