Marekani yataka Machar awekwe katika orodha nyeusi
Marekani imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limuweka kiongozi wa waasi wa Sudan Kusini, Riek Machar katika orodha nyeusi kwa tuhuma za kupanga njama ya kuipindua serikali ya Rais Salva Kiir.
Tayari Marekani imesambaza rasimu ya azimio hilo kwa wanachama 15 wa Baraza la Usalama ikizitaka ziunge mkono hoja hiyo ya kuwekewa vikwazo Machar pamoja na maafisa wengine wawili wa ngazi za juu wa Sudan Kusini.
Mbali na Machar, Marekani pia inataka kuwekwa katika jalada jeusi Mkuu wa Vikosi vya Majeshi ya Sudan Kusini Jenerali Paul Malong na Waziri wa Habari wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika, Michael Makuei.
Iwapo azimio hilo litapasishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, basi watatu hao watawekewa vikwazo vya usafiri mbali na kuzuiliwa mali zao.
Machar ambaye mara ya mwisho aliripotiwa kwamba yuko mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake, hivi majuzi alinukuliwa akisema hana wasi wasi kuwa atarejea nchini mwake hivi karibuni akisisitiza kwamba Rais Salva Kiir ndiye aliyeanzisha mapigano mapya mjini Juba mwezi Julai mwaka huu, kwa kuwa anaogopa kufanyika uchaguzi huru, ulio wazi na wa kidemokrasia.
Marekani inamtuhumu Jenerali Malong kuwa alipanga njama iliyogonga mwamba ya mauaji dhidi ya Machar Julai mwaka huu, huku ikimtuhumu Makuei kuwa aliratibu na kuhusika katika shambulizi dhidi ya ofisi ya Umoja wa Mataifa katika jimbo la Jonglei Aprili 2014, ambapo askari 3 wa UN waliuawa mbali na raia 140.
Pendekezo la Marekani limetolewa siku chache baada ya kuuawa watu 15 katika makabiliano mapya kati ya jeshi la serikali na waasi nchini Sudan Kusini, katika kijiji cha Adaab el Bahr, Jimbo la Unity, karibu na mpaka wa pamoja na Sudan.