Obama: Miaka minane ya mafanikio na kufeli
https://parstoday.ir/sw/news/world-i23323-obama_miaka_minane_ya_mafanikio_na_kufeli
Katika hotuba yake ya mwisho kama rais wa Marekani, Barack Obama amefafanua kuhusu mafanikio ya miaka minane ya serikali yake huku akionya kuhusu matatizo ambayo nchi hiyo itakabiliana nayo katika siku za usoni.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Jan 12, 2017 04:20 UTC

Katika hotuba yake ya mwisho kama rais wa Marekani, Barack Obama amefafanua kuhusu mafanikio ya miaka minane ya serikali yake huku akionya kuhusu matatizo ambayo nchi hiyo itakabiliana nayo katika siku za usoni.

Akizugumza Jumatano mjini Chicago, Obama alizungumzia kuboreka uchumi, mapatano ya nyuklia na Iran, maelewano na Cuba na kuuawa kinara wa Al Qaeda, Bin Laden, kuwa kati ya mafanikio makubwa ya serikali yake inayoondoka. Katika upande wa pili Obama ametaja nukta ambazo alifeli katika utawala wake kuwa ni pamoja na kuendelea malumbano katika jamii, ubaguzi wa rangi, ukosefu wa uadilifu wa kijamii, mfumo dhaifu wa elimu na afya Marekani.

Eric Simon, mchambuzi wa masuala ya kisiasa anasema hivi kuhusu hotuba ya Obama: "Katika hotuba yake ya mwisho, rais wa Marekani amejaribu kidhahiri kubanisha jitihada na malengo yake katika miaka minane aliyokuwa Ikulu ya White House. Lakini ametoa tahadhari kwa Wamarekani kuhusu namna Donald Trump, mrithi wa kiti chake anavyohatarisha demokrasia nchini humo. Kimsingi Obama amewaonya Wamarekani kuhusu urais wa  Trump na kuwataka wajitayarishe kukabiliana naye." Miaka minane ya urais wa Barack Obama imekuwa na panda shuka nyingi kwa Wamarekani na kwa watu wa dunia nzima.

Wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan

Wakati Obama alipochukua hatamu za uongozi, Marekani ilikuwa katika mgogoro mkubwa wa kiuchumi huku askari wa nchi hiyo wakiwa vitani Afghanistan na Iraq. Aidha jamii ya Marekani ilikuwa ikikabiliwa na matatizo makubwa kama vile ukosefu wa ajira, mashirika kufilisika kifedha, ufa mkubwa katika ya pato la juu na la chini, ukosefu wa uadilifu wa kijamii  na kadhalika. Ni katika mazingira kama haya ndio Obama akaja na nara ya 'Mabadiliko' na 'Sisi Tunaweza' na kwa kupandia wimbi la Wamarekani kutaka mabadiliko, aliweza kuingia katika Ikulu ya White House. Hivi sasa miaka minane baada ya utawala wa Obama, ni wazi kuwa amefanikiwa katika baadhi ya sekta lakini mafanikio hayo ni machache na duni sana ikilinganishwa na namna alivyofeli na kushindwa kutekeleza ahadi zake. Katika uga wa kiuchumi, hata kama Obama  alifanikiwa kupunguza kina cha mgogoro wa kiuchumi, lakini hakuweza kuzuia kufilisika mashirika mengi. Aidha katika sera zake za nidhamu ya kifedha, alipelekea deni la serikali kuu kuongezeka maradufu huku akishindwa kuleta bajeti yenye mlingano jambo ambalo lilipelekea shughuli za serikali kufungwa kwa muda, hii ikiwa ni mara ya pili katika historia ya Marekani jambo kama hilo kushuhudiwa.

Aidha pamoja na kuidhinishwa mpango wa bima ya afya maarufu kama Obamacare ambao ulitajwa kuwa mabadiliko makubwa zaidi ya kijamii Marekani katika nusu karne iliyopita, jamii ya Marekani haikuweza kunufaika kikamilifu na mpango huo.

Aidha katika kipindi cha urais wa Obama, kulishuhudiwa kuongezeka ufa mkubwa baina ya mshahara mkubwa zaidi na mdogo zaidi. Katika miaka minane ya Obama ubaguzi wa rangi ulidhihirisha sura yake kwa ukatili mkubwa na ukandamizaji wa watu wenye asili ya Afrika na kupelekea kuibuka maandamano makubwa katika barabara za nchi hiyo. Obama pia alishindwa kukabiliana na utumizi wa bunduki miongoni mwa raia na hakuweza pia kuleta mabadiliko yanayofaa katika sheria za uhamiaji nchini humo.

Wamarekani weusi walikandamizwa zaidi wakati wa utawala wa Obama

Nasser Fayyaz, mtaalamu wa masuala ya nchi za Magharibi katika mahojiano na Televisheni ya Sky News amesema katika hotuba yake ya kuaga, Obama alijaribu kubainisha zaidi mafanikio ya ndani ya nchi huku akijizuia kuzungumza kwa urefu kuhusu masuala ya kimataifa.

Katika uga wa kimataifa, Obama alipata mafanikio na pia kufeli katika masuala mengi. Kama tulivyotangulia kusema, Obama ametaja mapatano ya nyuklia na Iran, maelewano na Cuba na kuuawa bin Laden kuwa mafanikio ya utawala wake. Lakini alifeli katika mambo mengi katika uga wa kimataifa. Kwa mfano wakati wa utawala wa Obama kuliibuka msuguano mkubwa baina ya Marekani na Russia. Aidha Obama alishindwa kukabiliana na tishio la ugaidi na pia anatuhumiwa kuanzisha kundi la kigaidi la ISIS au Daesh.

Obama ambaye katika miezi ya awali ya utawala wake alipokea  Tunzo ya Amani ya Nobel, hakuweza kupunguza sera za kivita na kijeshi za Marekani. Si hayo tu bali hata alitoa amri ya kutumika ndege zisizo na rubani kutekeleza hujuma katika nchi za Kiislamu ambapo idadi kubwa ya raia wasio na hatia waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Abbad Kadhim, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema udiplomasia mbaya zaidi wa Marekani Mashariki ya Kati ulijiri wakati wa serikali ya Obama.

Kwa msingi huo tunaweza kusema kuwa, Obama alifeli zaidi kuliko alivyofanikiwa katika utawala wake. Ni kwa sababu hii ndio maana katika uchaguzi wa rais, Hillary Clinton aliyeonekana kama mwendelezaji wa sera za Obama akashindwa na Donald Trump aliyeahidi kuchukua mkondo tafauti.