Iran yapendekeza mazungumzo na nchi za Kiarabu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i25362-iran_yapendekeza_mazungumzo_na_nchi_za_kiarabu
Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Mohammad Javad Zarif amependekeza kuundwa jukwaa la pamoja na nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kwa lengo la kutafutia suluhisho matatizo yaliyopo katika eneo.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Feb 19, 2017 10:53 UTC
  • Iran yapendekeza mazungumzo   na nchi za Kiarabu

Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Mohammad Javad Zarif amependekeza kuundwa jukwaa la pamoja na nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kwa lengo la kutafutia suluhisho matatizo yaliyopo katika eneo.

Akizungumzao leo Jumapili katika Mkutano wa Usalama wa Munich, Zarif amesema nchi za Ghuba ya Uajemi zinapaswa kuondoa hali ya sasa ya migawanyiko na wasiwasi na kuelekea upande wa maelewano ya kieneo. Amesema hatua ya kwanza ya kufikia maelewano ni kuwepo jukwaa la mazungumzo.

Akihutubu katika mkutano huo wa kila mwaka wa wanadiplomasia wa ngazi za juu duniani, Zarif ametoa wito kwa nchi za Kiarabu kushirikiana na Iran kutatua hali ya wasiwasi na machafuko katika eneo la Asia Magharibi. Wiki iliyopita Rais Hassan Rouhani wa Iran alizitembelea Oman na Kuwait kuboresha uhusiano ikiwa ni safari yake ya kwanza katika Ghuba ya Uajemi tokea aingie madarakani mwaka 2013.

Akiwa mjini Munich pia, Zarif alikosoa vikali kufadhiliwa idiolojia ya ukufurishaji ambayo mizizi yake ni Saudi Arabia na ambayo imekuwa chimbuko la makundi ya kigaidi kama vile ISIS na Al Qaeda.

Mohammad Javad Zarif

Kuhusu mgogoro wa Asia Magharibi, Zarif amesema migogoro ya Iraq, Syria, Yemen na Bahrain haina suluhisho la kijeshi bali njia pekee ya kuitatua ni kupitia mazungumzo ya kisiasa yenye kuhusisha pande zote husika.

Aidha katika hotuba yake Zarif amesema Iran haitishwi hata kidogo na vitisho vya Marekani na kwamba itatoa jibu chanya kwa wenye kuiheshimu Jamhuri ya Kiislamu.