Kimbunga chasababisha maafa na hasara kisiwani Madagascar
Kimbunga cha Enawo kimesababisha vifo vya watu watano huku makumi ya maelfu ya wengine wakiachwa bila makao katika kisiwa cha Madagascar.
Afisi ya Taifa ya Kupambana na Majanga huko Madagascar (BNGC) imesema kuwa, watu zaidi ya elfu 10 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na athari za kimbunga hicho katika kipindi cha saa 48 zilizopita.
Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa, maelfu ya watu wamehamishwa kutoka wilaya ya Ampefiloha katika mji mkuu Antananarivo na kupelekwa katika uwanja wa michezo nyanda za juu.
Kitengo cha huduma za dharura cha Madagascar kimeziomba shule, maeneo ya ibada na kumbi za mikutano kuwahifadhi raia wote walioathiriwa na kimbunga hicho.
Nalo shirika la Msalaba Mwekundu limeonya kuwa, huenda athari zaidi za janga hilo la kimaumbile zikashuhudiwa katika siku zijazo.
Itakumbukwa kuwa, mwaka 2012, kimbunga cha Irina na tufani ya Giovanna vilisababisha vifo vya watu zaidi ya 100 nchini Madagascar.