Apr 16, 2017 02:51 UTC
  • Waislamu nchini Ufaransa waandamana kulalamikia kufungwa misikiti kadhaa

Waislamu nchini Ufaransa wameandamana kulalamikia siasa za chuki dhidi ya Uislamu na kufungwa misikiti kadhaa ndani ya nchi hiyo, kunakofanywa na serikali.

Mamia ya Waislamu wa mji wa Montfermeil katika viunga vya Paris, mji mkuu wa nchi hiyo, wameandamana mbele ya msikiti wa eneo hilo wakilalamikia hatua ya serikali kufunga msikiti wao na kuwazuia kusali swala ya jamaa ndani ya msikiti huo. Katika maandamano hayo ya kulalamikia siasa za chuki dhidi ya dini yao, Waislamu wa nchi hiyo wamebeba mabango yenye jumbe kama vile 'Misikiti Haifai Kufungwa' na 'Hatuna Mahala pa Kutekelezea Ibada.'

Jamii ya Waislamu Ufaransa wakiandamana kulaani ukandamizaji dhidi yao

Kabla ya hapo serikali ya Ufaransa na kwa kisingizio cha baadhi ya misikiti kutofungamana na sheria za usalama, ilifunga misikiti kadhaa na hivyo kuwafanya Waislamu kukosa mahala pa kuswalia. Mwanzoni mwa mwezi huu pia Waislamu wa eneo la Clichy, kaskazini mwa jiji la Paris, walilazimika kuswali swala ya Ijumaa nje ya jengo ambalo lilikuwa limefungwa na serikali ya mji huo ambalo awali lilikuwa likitumiwa na Waislamu hao kama msikiti.

Waislamu Ufaransa wakiswali barabarani kufuatia misikiti yao kufungwa

Hatua ya kufungwa kwa jengo hilo iliwanyima mamia ya watoto wa Kiislamu fursa ya kuendelea na masomo yao ya lugha ya Kiarabu na masomo mengine ya dini hiyo ambapo kufuatia hatua hiyo sasa hawataweza tena kuendelea na masomo yao katika eneo hilo. Inafaa kuashiria kuwa, karibu Waislamu milioni tano wanaishi nchini Ufaransa, hata hivyo kutokana na uhaba wa misikiti, wanalazimika kusalia mabarabarani, suala ambalo limegeuka na kuwa la kawaida.

Tags