Mar 11, 2016 16:24 UTC
  • Waislamu Marekani wakosoa chuki ya Warepublican dhidi yao

Waislamu nchini Marekani, wamesema kuwa maneno ya chuki dhidi ya dini tukufu ya Kiislamu yanayotolewa na viongozi wa chama cha Republican, ndiyo sababu ya kuongezeka hujuma na mashambulizi dhidi ya Waislamu nchini humo.

Taarifa iliyotolewa jana na viongozi wa jumuiya za Waislamu nchini Marekani mbele ya waandishi wa habari mjini Washington imemtaka Donal Trump, anayewania kuteuliwa na chama cha Republican kugombea urais nchini Marekani, kuwaomba radhi Waislamu kutokana na matamshi yake ya hivi karibuni yaliyojaa chuki dhidi yao. Itakumbukwa kuwa Jumatano usiku wakati akizungumza na kanali ya televisheni ya CNN, Trump alisema kuwa Uislamu unachafua sura ya Marekani. Nihad Awad, Mkurugenzi wa Baraza la Mahusiano la Kiislamu nchini Marekani amesema kuwa, Trump lazima awaombe radhi Waislamu ambao baadhi yao wanahudumu jeshini, kama ambavyo pia kuna madaktari Waislamu wanaookoa maisha ya mamilioni ya Wamarekani na pia kuna maafisa wa ngazi tofauti serikalini wanaowahudumia raia. Aidha amesisitiza kuwa, mgombea huyo wa nafasi ya urais kwa tiketi ya chama cha Republican anatakiwa kuwaomba radhi wanawake Waislamu ambao kutokana na kuvaa kwao vazi la Kiislamu la hijabu, wananyanyasika na kutengwa katika idara za serikali na mashuleni nchini Marekani. Kabla ya hapo pia jumuiya za Kiislamu nchini Marekani zilikuwa zimetahadharisha kwamba, matamshi ya kichochezi ya Donald Trump, yanawaweka hatarini Waislamu nchini humo.

Tags