Macron ashinda uchaguzi wa rais wa Ufaransa
https://parstoday.ir/sw/news/world-i28812-macron_ashinda_uchaguzi_wa_rais_wa_ufaransa
Emmanuel Macron mgombea huru wa kiti cha urais wa Ufaransa amemshinda mpinzani wake wa mrengo mkali wa kulia Marine Le Pen kwa kupata asilimia 66.1 ya kura zilizopigwa katika duru ya pili ya uchaguzi na hivyo kupata fursa ya kuwa rais mpya wa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 08, 2017 08:31 UTC

Emmanuel Macron mgombea huru wa kiti cha urais wa Ufaransa amemshinda mpinzani wake wa mrengo mkali wa kulia Marine Le Pen kwa kupata asilimia 66.1 ya kura zilizopigwa katika duru ya pili ya uchaguzi na hivyo kupata fursa ya kuwa rais mpya wa nchi hiyo.

Macron aliye na umri wa miaka 39 amemshinda mpinzani wake huyo wa chama cha National Front aliyepata asilimia 33.9 ya kura na hivyo kuwa rais aliye na umri mdogo zaidi kuwahi kuongoza katika historia ya Ufaransa. Kwa kweli ushindi wa Macron katika duru ya pili ya uchaguzi ulitarajiwa kwa kutilia maanani kwamba vyamba karibu vyote vya mrengo wa wastani kulia, wastani kushoto na kwa ufupi vyama vikuu vya Ufaransa vilimuunga mkono kwenye duru hiyo. Wakati huohuo tahadhari za mara kwa mara zilizokuwa zikitolewa na wanasiasa mashuhuri wa Ufaransa kuhusiana na matokeo mabaya na hatari ya kuchaguliwa Marine Le Pen zilichangia pakubwa katika kuwashawishi Wafaransa wampigie kura Macron. Kwa kadiri kwamba tunaweza kusema kuwa ushindi wa Macron ni ushindi wa Wafaransa wale ambao wamekuwa wakiunga mkono nchi hiyo kuendelea kubakia kuwa mwanachama wa Umoja wa Ulaya na vilevile siasa za hivi sasa za serikali ya nchi hiyo katika ngazi za kitaifa na kimataifa.

Macron baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa hivi karibuni

Kwa msingi huo tunaweza kutabiri kwamba serikali ijayo ya Ufaransa itaendelea kutekeleza sera zinazotekelezwa na serikali ya sasa ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais François Hollande. Na hasa tukitilia maanani kwamba Macron mwenyewe huko nyuma aliwahi kuwa msoshalisti na waziri katika serikali ya kisoshalisti ya nchi hiyo hadi mwaka 2014. Kuhusu siasa za kigeni Macron ni muungaji mkono mkubwa wa Umoja wa Ulaya katika hali ambayo mpinzani wake katika uchaguzi uliopita Marine Le Pen, ni mtaifa mwenye misimamo mikali ya kuchupa mipaka ambaye alikuwa na lengo la kuiondoa Ufaransa katika umoja huo. Hata hivyo Macron anataka kufanyike maadhi ya marekebisho ya kimsingi katika umoja huo, jambo ambalo linakubaliwa pia na viongozi wa ngazi za juu wa umoja huo kwa ajili ya kuufanya uendelee kudumu na kuwa na maana katika mazingira ya hivi sasa.

Marine Le Pen aliyeshindwa na Macron

Wakati huohuo Macron anataka kuimarishwa kwa nafasi ya Ufaransa katika shirika la kijeshi la nchi za Magharibi Nato. Hata kama tayari amempongeza kwa ushindi wake nchini Ufaransa lakini bila shaka ushindi wa Macron si habari njema kwa Rais Donald Trump wa Marekani kwa kutilia maanani kwamba alikuwa akimuunga mkono waziwazi mpinzani wake Marine Le Pen katika mchuano wa uchaguzi huo kutokana na kuwa alikuwa na fikra zinazofanana na zake. Katika upande wa pili, ushindi wa Macron ni habari njema kwa viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya na hasa Angela Markel wa Ujerumani ambaye alikuwa kimuunga mkono waziwazi Macron kabla ya kufanyika duru ya pili ya uchaguzi huo. Kwa sasa viongozi wa nchi hizo wanaamini kwamba ushirikiano wa serikali ya Ufaransa katika Umoja wa Ulaya utaendelea kuwepo kwa uchache hadi mwishoni mwa uongozi wa Macron.

Uchaguzi wa mwaka huu wa rais wa Ufaransa

Katika upande wa ndani, mabadiliko makubwa yanatazamiwa kufanyika katika nyanja za uchumi na masuala ya kijamii na kijeshi. Kwa kutilia maanani uzoefu wake kama waziri wa zamani wa uchumi wa nchi hiyo na vilevile masomo yake ya masuala ya benki na uwekezaji, Macron ni mmoja wa waungaji mkono wakubwa wa uchumi wa soko huru na moja ya mipango yake ni kuhakikisha kwamba matakwa ya Kamisheni ya Ulaya ya kupunguza nakisi ya bajeti ya nchi hiyo hadi asilimia 3 ya patojumla la ndani, yanafikiwa. Katika upande wa kijamii pia, mapambano dhidi ya ukosefu wa ajira ambalo ni tatizo kubwa zaidi linaloikabili Ufaransa kwa sasa, ni miongoni mwa changamoto muhimu zinazomsubiri rais huyo mpya. Rais wa kisoshalisti François Hollande hakufanikiwa pakubwa kutatua tatizo hilo katika kipindi cha uongozi wake. Hii ni katika hali ambayo suala la wakimbizi ni changamoto nyigine muhimu inayomsubiri Macron, pamoja na kuwa tayari ameshatangaza mfungamano wake na Ujerumani na Umoja wa Ulaya kuhusiana na jambo hilo.

Mkataba wa Schengen kati ya nchi za Umoja wa Ulaya

Ama kuhusiana na suala la usalama, changamoto nyingine kubwa inayoikabili Ufaransa ni kuendelea kuwepo kwa tishio la ugaidi, suala ambalo limepewa kipaumbele cha kwanza katika serikali mpya ya Macron. Mipango inayopewa umuhimu kuhusu suala hilo ni ya kimuundo. Mipango hiyo inajumuisha kuimarishwa vikosi vya usalama na hasa polisi na kubuniwa idara zitakazokuwa zikitekeleza majukumu yao chini ya ofisi ya rais wa nchi kwa ajili ya kutaribu vyema shughuli zote za vikosi vya usalama katika kupambana na ugaidi. Kinyume na alivyokuwa Marine Le Pen ambaye amekuwa akisisitiza kuimarishwa  usalama na kudhibitiwa zaidi mipaka ya nchi hiyo, Macron anasisitiza umuhimu wa kulindwa mkataba wa Schengen na kudumishwa siasa za mipaka iliyo wazi kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.