HRW yasikitishwa na hatua ya UNESCO ya kufanya kikao Saudia
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa, limesikitishwa na hatua ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ya kufanya kongamano la kimataifa la asasi zisizo za kiserikali huko nchini Saudi Arabia.
Taarifa ya Human Rights Watch iliyotolewa jana sambamba na kuonyesha masikitiko yake kwa hatua ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) ya kufanya kongamano hilo la kimataifa la jumuiya zisizo za kiserikali katika mji mkuu wa Saudia Riyadh imetangaza kuwa, faili la Saudia kuhusiana na wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu linatisha; kwani utawala wa Aal Saud umeendelea kuwatesa na kuwadhalilisha wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu.
Sehemu nyingine ya taarifa ya Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch imeeleza kuwa, baadhi ya asasi za Umoja wa Mataifa hivi karibuni zimechukua maamuzi ambayo yako mbali kabisa na ukweli wa mambo kuhusiana na Saudi Arabia ambayo ina faili la kutisha kuhusiana na ukiukaji wa haki za binadamu.
Human Rights Watch imesema bayana kwamba, kufanyika nchini Saudia kongamno la jumuiya zisizo za kiserikali ni sawa na kupigwa kibao cha uso watu ambao wako gerezani hivi sasa nchini humo kwa kosa la kuanzisha jumuiya huru nchini humo.
Ikumbukwe kuwa juma lililopita Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO) lilifanya kongamano lake la saba la jumuiya za kimataifa zisizo za kiserikali mjini Riyadh likiwa na nara ya "Vijana na Taathira Yao Katika Jamii, hatua ambayo imekosolewa kieneo na kimataifa hasa kutokana na rekodi mbaya ya nchi hiyo ya Kiarabu ya kukiuka haki za binadamu.