Polisi ya Ufaransa yawatia mbaroni wanawake wa Kiislamu waliojistiri kwa hijabu
Polisi ya Ufaransa imewatia nguvuni wanawake 10 wa Kiislamu kwa kosa la kuvaa vazi la staha la hijabu katika mji wa Cannes.
Duru za habari nchini humo zimearifu kwamba, wanawake hao walitiwa mbaroni Ijumaa ya jana kwa kosa la kuvaa vazi hilo la Kiislamu aina ya burqini katika pwani ya mji wa Cannes. Burqini ni vazi la kujisitiri wanawake wa Kiislamu wakati wa kuogelea ambalo aghlabu hutumiwa na wanawake hao barani Ulaya.
Marufuku ya utumiwaji wa vazi hilo, ilikabiliwa na ukosoaji mkubwa kutoka kwa Waislamu na wanaharakati wa kidini ndani na nje ya Ufaransa. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, polisi wa Ufaransa wameshadidisha ulinzi katika mji wa Cannes ambao ni mwenyeji wa tamasha la kimataifa la filamu ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya askari mjini hapo. Tamasha la kimataifa la filamu mjini Cannes litafikia tamati siku ya Jumapili.
Mwaka jana Waziri wa Elimu wa nchi hiyo Najat Vallaud-Belkacem alikosoa hatua ya Waziri Mkuu wa wakati huo Manuel Valls ya kupiga marufuku vazi hilo la stara la kuogelea kwa ajili ya wanawake wa Kiislamu akisema kuwa, baadhi ya nukta zilizomo katika marufuku hiyo zinawakandamiza moja kwa moja wanawake katika hali ambayo serikali haitakiwi kuwalazimisha wananchi kuachana na dini zao.