Jun 08, 2017 06:46 UTC
  • Trump awalaumu na kuwakejeli mashahidi wa mashambulio ya Tehran

Katika hali ambayo dunia nzima inaendelea kutoa mkono wa pole na kutuma salamu za rambirambi kufuatia mashambulio pacha ya kigaidi yaliyotokea jana hapa mjini Tehran, Rais Donald Trump wa Marekani ametoa ujumbe unaoonekana kuwalaumu na kuwakejeli mashahidi waliouawa katika hujuma hizo.

Trump amekariri madai yake yasio na msingi kuwa Tehran ni muungaji mkono wa ugaidi na kwamba taifa la Iran limekuwa mhanga wa harakati linazounga mkono.

Hii ni licha ya kuwa genge la kigaidi na kitakfiri la Daesh limekiri kuhusika na mashambulio hayo yaliyosababisha watu 16 kuuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa.

Trump kwa upande mmoja amedai kuwasikitikia wahanga wa mashambulio hayo ya kigaidi ya Tehran na kwa upande mwingine kusema: "Tunasisitiza kuwa, mataifa yanayounga mkono ugaidi, yapo katika hatari ya kuwa wahanga wa uovu wanayoufadhili." 

Maafisa usalama wa Iran wakilinda doria baada ya hujuma za jana Tehran

Hii ni katika hali ambayo, Mratibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa hapa nchini na Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya wamelaani mashambulio hayo.

Kadhalika hapo jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilikaa kimya kwa muda wa dakika moja kwa heshima ya watu waliouawa katika mashambulio ya kigaidi yaliyotokea leo hapa mjini Tehran.

Tags