Korea Kaskazini yasherehekea majaribio ya bomu la nyuklia
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34025-korea_kaskazini_yasherehekea_majaribio_ya_bomu_la_nyuklia
Sherehe kubwa zimefanyika nchini Korea Kaskazini kuwaenzi wanasayansi waliofanikisha majaribio makubwa zaidi ya bomu la nyuklia kuwahi kufanyika nchini humo.
(last modified 2024-06-10T09:25:34+00:00 )
Sep 07, 2017 07:56 UTC
  • Korea Kaskazini yasherehekea majaribio ya bomu la nyuklia

Sherehe kubwa zimefanyika nchini Korea Kaskazini kuwaenzi wanasayansi waliofanikisha majaribio makubwa zaidi ya bomu la nyuklia kuwahi kufanyika nchini humo.

Wananachi walimiminika katika mji mkuu, Pyongyang Jumatano huku wakishangilia wanasayansi waliokuwa ndani ya basi katika barabara kuu za mji huo ambapo makumi ya maelfu ya watu walijumuika katika Uwanja wa Kim II-Sung kuwapongeza.

Siku ya Jumapili Korea Kaskazini ilifanyia jaribio kwa mafanikio bomu la nyuklia aina ya Hydrogen lenye uwezo mkubwa wa uharibifu  na likiwa ni jaribio la sita la aina hii kufanywa na Pyongyang. Jaribio hilo lilisababisha mtetemeko wa ardhi wenye ukubwa wa 6.3 kwa kipimo cha rishta.

Kombora la Balistiki la Korea Kaskazini

Pyongyang imefanya jaribio hilo licha ya taharuki kutanda katika Peninsula ya Korea na vikwazo vya kila mara vya Marekani na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi yake.

Serikali ya Korea Kaskazini inasisitiza kuwa, inalazimika kumiliki silaha za nyuklia kwa lengo la kujihami kutokana na vitisho vya Marekani vya kuivamia kijeshi kwa mabomu ya nyuklia. Marekani imekuwa ikifanya mazoezi ya kijeshi mara kwa mara na Korea Kusini, mazoezi ambayo Korea Kaskazini inayaona kuwa tishio.