Mauaji ya kimbari ya Waislamu wa Myanmar
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34083-mauaji_ya_kimbari_ya_waislamu_wa_myanmar
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekemea tena mauaji ya kimbari yanayofanyika nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya na kusema kuwa: Jamii ya Kimataifa inapaswa kuchukua hatua haraka bila ya kucheleza zaidi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 08, 2017 17:16 UTC

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekemea tena mauaji ya kimbari yanayofanyika nchini Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya na kusema kuwa: Jamii ya Kimataifa inapaswa kuchukua hatua haraka bila ya kucheleza zaidi.

Muhammad Javad Zarif alisema jana katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Twetter kwamba: "Hakuna sababu yoyote ya jamii ya kimataifa kuruhusu mauaji ya kimbari yaendelee kufanyika dhidi ya Waislamu wa Rohingya."

Wimbi jipya la mauaji na jinai za jeshi na Mabudha wa Myanmar dhidi ya Waislamu nchini humo pia limezilazimisha hata taasisi zinazodai kutetea haki za binadamu kupaza sauti ya kupinga ukatili huo, japokuwa hakuna hatua ya maana iliyochukuliwa kukomesha jinai hizo. Wale ambao jana walimtunuku Tuzo ya Amani ya Nobel, Aung San Suu Kyi, Mshauri Mkuu wa Serikali ya Myanmar ambaye pia ndiye Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo sasa wamekhitari kufyata ulimi na kutazama kwa macho ukatili na mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa Rohingya. Siku chache zilizopita San Suu Kyi alikana kutokea mauaji ya kimbari nchini Myanmar licha ya ushahidi mwingi unaothibitisha suala hilo na hivyo akatetea kivitendo harakati za jeshi la nchi hiyo katika mkoa wenye Waislamu wengi wa Rakhine. 

Hata watoto wadogo hawakusalimika Myanmar

Waislamu wa Rongya nchini Myanmar wanatambuliwa kuwa ndiyo jamii ya waliowachache inayodhulumiwa na kufanyiwa ukatili zaidi katika dunia ya sasa. Tunapotupia jicho kwa haraka ripoti chache zinazorushwa hewani kutoka katika jimbo la Rakhine inatubainikia wazi picha ya jinai dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari yanayoendelea kufanyika nchini Myanmar dhidi ya Waislamu hao. Vitendo vya kuchomwa moto watu na milki, kukatwa vichwa na kubakwa na kunajisiwa wanawake na wasichana vinavyofanywa dhidi ya Waislamu wa Myanmar haviwezi kuhalalishwa kwa njia yoyote ile. Vilevile uzembe na misimamo dhaifu ya jamii ya kimataifa, nchi jirani, Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) inaakisi "kifo cha ubinadamu".

Jeshi linahusika moja kwa moja kuua Waislamu Myanmar

Inawezekana sana kukomesha mauaji ya kimbari yanayofanyika Myanmar, lakini inasikitisha kuona kuwa, mitazamo ya kisiasa inayotawala taasisi za kimataifa zinazosimamia amani ya dunia inakwamisha suala hilo. Hali hii imelipa jeshi la Myanmar fursa ya kuendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa Rohingya huku Aung San Suu Kyi akiendelea kunyamaza kimya mbele ya mauaji hayo. Hali hii inazilazimisha taasisi za kutetea haki za binadamu kuwa makini zaidi katika kuainisha sifa za watu wanaostahiki kupewa Tuzo ya Amani ya Nobel katika siku za usoni. Kwa hakika mauaji yanayoendelea kufanyika huko Myanmar mbele ya macho na kimya cha Aung San Suu Kyi anayedai kutetea haki za binadamu, yameonesha tena jinsi suala hilo la haki za binadamu linavyotumiwa kama wenzo tu wa kutimiza malengo na maslahi ya watu au kundi makhsusi.

Aung San Suu Kyi, msindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel !!

Kama tulivyosema mwanzoni ,mauaji yanayofanyika nchini Myanmar dhidi ya Waislamu hayawezi kuhalalishwa kwa njia yoyote ile na kwa msingi huo Umoja wa Mataifa na hasa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) zinapaswa kuchukua hatua za haraka za kukomesha mauaji hayo ya kizazi.