Ufaransa: Kutiwa mbaroni Salah Abdeslam ni pigo kubwa kwa Daesh
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ufaransa, Bernard Cazeneuve amesema kuwa, kutiwa mbaroni Salah Abdeslam, mshukiwa mkuu wa mashambulizi ya umwagaji damu mkubwa ya mwezi Novemba mwaka jana jijini Paris, Ufaransa na kusababisha makumi ya watu kuuawa, ni pigo kubwa kwa kundi la kigaidi la Daesh barani Ulaya.
Cazeneuve amesema, kutiwa mbaroni Abdeslam siku ya Ijumaa mjini Brussels, Ubelgiji, ni pigo kubwa kwa kundi hilo ambalo lilitangaza kuhusika katika hujuma hizo. Ameongeza kuwa, serikali ya Paris imeazimia kuzuia kila aina ya jinai na mashambulizi ya kigaidi nchini humo. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Ufaransa amesisitiza kuwa, Salah Abdeslam anapaswa kupandishwa kizimbani ili kujibu tuhuma dhidi yake. Jumamosi ya jana, Baraza la Usalama na Ulinzi nchini Ufaransa, lilifanya kikao kwa minajili ya kuchunguza faili la vita dhidi ya ugaidi, kikao ambacho kilihudhuriwa na Rais François Hollande, wa nchi hiyo. Kikao hicho kimefanyika ikiwa ni siku moja tu tangu kutiwa mbaroni Salah Abdeslam, mshukiwa mkuu wa mashambulizi ya mjini Paris. Rais François Hollande ameonyesha kuridhishwa kwake na hatua ya kutiwa mbaroni mshukiwa huyo na kusisitizia udharura wa kuendelezwa mapambano dhidi ya mitandao yote ya kigaidi nchini Ufaransa.