Russia kufanya mazungumzo na Korea Kaskazini
https://parstoday.ir/sw/news/world-i34911-russia_kufanya_mazungumzo_na_korea_kaskazini
Afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema kuwa, Moscow imepanga kuanza mazungumzo ya kisiasa na Korea Kaskazini kwa ajili ya kupunguza mivutano na hofu katika rasi ya Korea.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 27, 2017 09:58 UTC
  • Russia kufanya mazungumzo na Korea Kaskazini

Afisa mmoja wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia amesema kuwa, Moscow imepanga kuanza mazungumzo ya kisiasa na Korea Kaskazini kwa ajili ya kupunguza mivutano na hofu katika rasi ya Korea.

Shirika la habari la Interfax la Russia limemnukuu afisa huyo wa wizara ya mambo ya nje ya nchi hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake akisema kuwa, mazungumzo baina ya Russia na Korea Kaskazini yamepangwa kufanyika tarehe 29 mwezi huu wa Septemba.

Kabla ya hapo, afisa mmoja wa ubalozi wa Korea Kaskazini mjini Moscow alikuwa ameliambia shirika la habari la Interfax kwamba ujumbe wa kidiplomasia wa nchi yake uliwasili mjini Moscow jana Jumanne kwa mwaliko wa viongozi wa Russia.

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un

 

Mkurugenzi wa kitengo cha kudhibiti na kuzuia uenezaji silaha za nyuklia cha wizara ya mambo ya nje ya Russia kwa upande wake amesema, nchi yake inaamiliana kwa tahadhari na Korea Kaskazini katika jitihada za kutatua mgogoro wa rasi ya Korea.

Korea Kaskazini ilianza kujiimarisha kwa silaha za nyuklia tangu mwaka 1950 na harakati hizo zimepamba moto wakati wa kiongozi wa hivi sasa wa nchi hiyo, Kim Jong-un.

Tangu mwaka 2006 hadi hivi sasa, Korea Kaskazini imeshafanya majaribio sita ya nyuklia huku majaribio mawili yakiwa yamefanyika katika kipindi cha wiki tatu tu zilizopita.