Wamarekani zaidi ya milioni moja waunga mkono mpango wa kuuzuliwa Trump
Saini zaidi ya milioni moja zimekusanywa ndani ya siku kumi nchini Marekani katika kampeni ya kutaka kuondolewa madarakani Rais Donald Trump wa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na tovuti ya Axiod, kampeni hiyo inaendeshwa na Tom Steyer, bilionea na mfuasi mashuhuri wa chama cha Democratic cha nchi hiyo kupitia matangazo ya biashara na nyaraka kwa Wabunge.
Hadi kufikia sasa Wamarekani milioni 1, laki 1 na elfu 19,720 wametia sahihi zao kuunga mkono mpango huo wa kuondolewa madarakani Trump.
Steyer alianzisha kampeni hii Oktoba 20, kupitia tangazo la biashara akiwaasa wabunge wa Kongresi ya Marekani wamuuzulu Trump, kutokana na hatua zake zilizo dhidi ya wahamiaji, mfumo wa afya na mazingira.
Katika moja ya kanda za video alizotumia kwenye matangazo hayo ya biashara, mwekezaji huyo tajiri wa Marekani amesema: Trump ametufikisha katika nchi ya vita vya kinyuklia, amekiuka sheria na haki ndani ya FBI na pia amepokea pesa kutoka serikali za nje kwa njia isiyo ya halali.
Si vibaya kuashiria hapa kuwa, Januari mwaka huu, watu zaidi ya milioni moja nchini Uingereza walisaini ombi la malalamiko wakiitaka serikali ya nchi hiyo kufuta mwaliko wa Rais Donald Trump wa Marekani kwenda London kwa ajili ya kuonana na Malkia Elizabeth wa nchi hiyo.