Gallup: UKiwango cha maisha ya Wamarekani kimeshuka sana mwaka huu
Uchunguzi mpya uliofanywa na Taasisi ya Kimarekani ya Gallup unaonyesha kwamba, kiwango cha maisha ya Wamarekani kimeendelea kushuka mwaka huu wa 2017 na hivyo kuwafanya raia wa taifa hilo kuishi maisha magumu.
Kabla ya hapo gazeti la The Independent linalochapishwa mjini London, Uingereza liliutaja mwaka jana 2016 ambao ndani yake Wamarekani walishuhudia kampeni za uchaguzi zilizovutia hisia za walio wengi na kuibuka mzozo wa kisiasa nchini humo, sambamba na uchaguzi uliomuingiza madarakani Rais Donald Trump, kuwa mwaka mbaya sana kwa taifa hilo.
Aidha uchunguzi wa tasisi ya Gallup unaonyesha kwamba, kiwango cha maisha bora kimezidi kudidimia mwaka huu 2017 na kuwafanya raia wengi wa nchi hiyo waishi maisha magumu. Kwa mujibu wa taasisi hiyo, kupungua kiwango cha maisha bora, siasa mbovu na mienendo isiyofaa ya Rais Donald Trump ndio sababu kuu ya Wamarekani kutoridhishwa na serikali ya Washington hivi sasa. Uchunguzi huo umefanywa kwa kuwahoji zaidi ya watu laki moja na elfu 35 kuanzia tarehe Pili Januari hadi tarehe 30 Disemba mwaka huu ndani ya majimbo 50 ya Marekani.
Kukosekana usalama wa kimwili na kifedha, kukosa mahala pazuri pa kuishi, kukosekana usalama wa kazi na mahusiano kati ya watu wa familia na marafiki, ni vitu vilivyoulizwa katika uchunguzi huo. Aidha kwa mujibu wa uchunguzi huo, kiwango cha maisha bora cha raia wa Marekani kimepungua na kufikia asilimia 61.5 ambapo mwaka jana 2016 kilikuwa asilimia 62.01 na kwamba mporomoko ni mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu mwaka 2008.