Russia: Marekani ni dola vamizi, halikualikwa nchini Syria
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa kuwepo wanajeshi wa Marekani katika ardhi ya Syria ni uvamizi na ni kinyume cha sheria.
Matamshi hayo ya Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia yametolewa baada ya James Mattis, Waziri wa Ulinzi wa Marekani kudai kuwa eti wanajeshi wa Marekani wako nchini Syria kwa idhini ya Umoja wa Mataifa. Lavrov amesema, madai hayo ya Marekani ni upotoshaji wa wazi na hayana msingi wowote.
Hivi sasa kuna wanajeshi wapatao 500 wa Marekani kinyume cha sheria ndani ya ardhi ya Syria kwa madai ya kupambana na kundi la kigaidi la Daesh. Hata hivyo hakuna kikao chochote cha Umoja wa Mataifa kilichoiruhusu Marekani kutuma wanajeshi wake nchini humo kama ambavyo pia serikali ya Syria si tu haikutoa idhini kwa Marekani kutuma wanajeshi wake nchini humo, bali hata imekuwa ikilalamikia vikali uvamizi wa dola hilo la kibeberu na kutojali kwake haki ya kujitawala nchi hiyo huru ya Kiarabu.
Mgogoro wa Syria ulianzishwa mwaka 2011 baada ya magaidi wanaoungwa mkono na Saudia, Israel, Marekani na waitifaki wao kukanyaga sheria zote za kimataifa na kuivamia Syria kutoka kona zote za dunia. Hata hivyo vikosi vya ulinzi vya Syria kwa kushirikiana na kambi ya muqawama vimeweza kubatilisha kabisa njama hizo kubwa za madola ya Magharibi na vibaraka wao.