Jaribio la mauaji ya Waziri Mkuu wa Uingereza lazimwa
Polisi ya Uingereza imetangaza kuwa, imezima jaribio la mauaji ya kigaidi dhidi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Theresa May.
Vyombo kadhaa vya habari ikiwemo televisheni ya Sky News na gazeti la The Sun vimetangaza kuwa, polisi ya Uingereza imezima jaribio hilo ambalo lilipangwa kutekelezwa kwa bomu la kujilipua ndani ya ofisi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo Theresa May, huko Downing Street kisha kumuua kwa kumpiga risasi kwa kutumia ghasia na hali na mchafukoge ambayo ingejitokeza baada ya shambulizi la bomu.
Duru za Uingereza zimesema polisi ya nchi hiyo na vyombo vya usalama vimekuwa vikifuatilia njama hiyo tangu wiki kadhaa zilizopita. Polisi pia imewatia nguvuni washukiwa wawili.
Awali Msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza alisema kuwa, polisi na vyombo vya upelelezi wa ndani vimezima majaribio 9 ya mauaji nchini humo katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.