El-Helbawy: Wanaowafitinisha Masuni na Mashia wana akili za kigomvi
Mjumbe wa Baraza la Taifa la Haki za Binaadamu nchini Misri, Kamal El-Helbawy amesema kuwa, wale wanaozusha fitna baina ya Waislamu wa Kisuni na Kishia, wana akili zilizojengeka juu ya ugomvi.
Dakta El-Helbawy ambaye pia ni msemaji wa harakati ya iliyopigwa marufuku ya Ikhwanul Muslimin, aliyasema hayo jana Jumamosi na kusisitiza kuwa, watu ambao wanafanya njama chafu za kuibua mifarakano baina ya Waislamu wa Kisuni na wenzao wa Kishia, ni watu ambao fikra na akili zao zimejengeka tu juu ya ugomvi na mapigano. Ameongeza kusema kuwa, lengo la adui wa Uislamu ni kuzusha mizozo ya kimadhehebu baina ya Suni na Shia. Amesisitiza kuwa, lengo halisi la adui katika njama hizo ni kuzuia kuimarika dini ya Kiislamu duniani na kwamba umefika wakati kwa Waislamu kuwa makini kutokana na malengo hayo machafu ya adui dhidi yao. Matamshi ya msomi huyo yametolewa katika hali ambayo, baadhi ya Waislamu wenye misimamo ya Kiwahabi wamekuwa wakieneza propaganda chafu dhidi ya Waislamu wa Kishia duniani, propaganda ambazo zimekuwa chanzo cha fitina na mauaji dhidi ya Waislamu wengine.