Mar 08, 2018 08:17 UTC
  • UN: Haki za binadamu zinakanyagwa katika nchi nyingi duniani

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, haki za binadamu zinatishiwa au kukanyagwa katika zaidi ya nchi 50 kote duniani.

Zeid Ra’ad al-Hussein ambaye alikuwa akihutubia kikao cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali ya haki za binadamu duniani hususan katika nchi kama Libya, Yemen, Ufilipino, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Myanmar, Venezuela na Syria na kusema hali ya haki za binadamu inatia wasiwasi zaidi katika maeneo hayo. 

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema katika ripoti yake ya kila mwaka iliyowasilishwa katika kikao hicho kwamba, wanasiasa ndio wasababishaji wakuu wa hali hiyo ya kutia wasiwasi. 

Zeid Ra’ad al-Hussein pia amekosoa vikali sera za nchi za Ulaya kuhusiana na wakimbizi.

Wakimbizi wanashambuliwa na kupigwa Ulaya badala ya kusaidiwa

Ripoti hiyo imeashiria hali ya kusikitisha ya Syria na kusema kuwa, mzingiro wa eneo la Ghouta Mashariki lenye raia karibu laki nne wanaoshikiliwa katika eneo hilo hauwezi kutetewa wala kuhalalishwa kwa njia yoyote ile. Eneo hilo la kistratijia lililoko karibu na mji mkuu wa Syria, Damascus linakaliwa kwa mabavu na makundi ya kigaidi yanayoungwa mkono na baadhi ya nchi za Magharibi kama Marekani na vilevile Saudi Arabia. Magaidi wamekuwa wakitumia eneo hilo kushambulia mji mkuu wa Syria kwa maroketi na kuua raia wasio na hatia. 

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu hali ya Waislamu wa Rohingya huko Myanmar na kusema kuwa, kuna viashiria vya kufanyika mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu hao.   

Tags