Mar 17, 2018 07:59 UTC
  • Umoja wa Mataifa watoa wito wa kusaidiwa wakimbizi Waislamu Warohingya

Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kukusanywa misaada kwa ajili ya kuwasaidia wakimbizi takribani milioni moja wa jamii ya Rohingya wa Myanmar ambao wako katika kambi za wakimbizi nchini Bangladesh sambamba na kuandaliwa mazingira ya Waislamu hao kurejea nchini kwao.

Umoja wa Mataifa umesema katika tangazo lake kwamba, panahitajika kiasi cha karibu dola bilioni moja kwa ajili ya misaada ya wakimbizi hao wa Kiislamu hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa 2018.

Filippo Grandi, Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) ametangaza kuwa, shirika hilo linatoa kipaumbele suala la kuwapatia misaada ya haraka wakimbizi Waislamu Warohingya katika kipindi hiki cha kuwadia msimu wa mvua na uwezekano wa kutokea mafuriko na maporomoko ya udongo.

Filippo Grandi, Mkuu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa 

Wakati huo huo, asasi mbalimbali za kieneo na kimataifa zimeendelea kutahadharisha kuhusiana na hali mbaya inayowakabili wakimbizi wa Kiislamuu wa Myanmar walioko nchini Bangladesh.

Hivi karibuni Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alielezea wasi wasi mkubwa alionao kwamba yumkini mauaji ya kimbari yamefanywa dhidi ya Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar tangu Agosti mwaka jana 2017.  

Maelfu ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar wameuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa, mbali na wengine zaidi ya laki saba kulazimishwa kukimbilia katika nchi jirani ya Bangladesh, tangu Agosti 25 mwaka jana, lilipoanza wimbi jipya la mashambulizi ya jeshi na Mabudha wenye misimamo mikali katika mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi nchi hiyo. 

Tags