IAEA: Iran inatekeleza ipasavyo makubaliano ya nyuklia
Kwa mara nyingine tena Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA umetoa ithibati kuwa serikali ya Tehran inatekelezwa barabara makubaliano ya nyuklia yaliyofikiwa kati yake na kundi la 5+1 Julai mwaka jana 2015.
Yukiya Amano, Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo aliyasema hayo jana pambizoni mwa Kongamano la Usalama wa Nyuklia mjini Washington baada ya kufanya mazungumzo na viongozi wa China, Russia, Marekani, Uingereza, Ufaransa na Umoja wa Ulaya kuhusiana na iwapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekengeuka mkondo wa miradi ya nyuklia kwa mujibu wa miongozo ya Utekelezaji wa Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) au la.
Amano amesema Iran si tu imetekeleza wajibu wake na kuheshimu makubaliano ya Vienna, bali pia imeonyesha uwazi wa hali ya juu wa kukaguliwa vituo vyake vya nyuklia, sambamba na Makubaliano ya Kuzuia Utengenezaji na Usambazaji Silaha za Nyuklia NPT. Mkurugenzi Mkuu wa IAEA ameongeza kuwa Iran inaendelea kutekeleza Protokali ya Ziada kwa muda tangu tarehe 16 Januari mwaka huu.
Ni vyema kuashiria hapa kuwa, Disemba mwaka jana, Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ilipitisha kwa kauli moja azimio la kufunga faili la nyuklia la Iran baada ya kubaini kwamba miradi ya nyuklia ya taifa hili ni ya amani na haijawahi kuchukua mkondo wa kijeshi. Wanachama 35 wa bodi hiyo walisema baada ya Iran kutoa majibu ya kuridhisha kuhusiana na miradi yake ya nyuklia, IAEA imeamua kufunga faili hilo lililofunguliwa miaka 12 iliyopita.