Korea Kusini yasisitiza wanajeshi wa Marekani waendelee kubaki nchini humo
Msemaji wa ofisi ya Rais wa Korea Kusini amesisitiza kuwa wanajeshi wa Marekani inapasa waendelee kubaki nchini humo.
Kim Eui-kyeom ameashiria mazungumzo ya amani na jirani wa Seoul, Korea Kaskazini na kueleza kwamba kwa vyovyote vile matokeo ya mazungumzo yatakavyokuwa Korea Kusini inataka wanajeshi wa Marekani waendelee kuwepo nchini humo na katika eneo la Peninsula ya Korea.
Kim Eui-kyeom ameongeza kuwa maudhui ya wanajeshi wa Marekani walioko nchini Korea Kusini inahusiana na umoja uliopo baina ya Seoul na Marekani na wala haina uhusiano wala mfungamano wowote na mikataba ya amani na suluhu kati ya Korea Kusini na Korea Kaskazini.
Msimamo huo umetoa mguso kwa vyombo vya habari vya Korea Kusini baada ya Moon Chung-in, mshauri wa rais wa nchi hiyo kutanabahisha kuwa endapo suluhu itafikiwa baina ya Korea mbili, itakuwa vigumu kuhalalisha kuendelea kuwepo wanajeshi wa Marekani katika nchi hiyo.
Kuna askari wapatao 29,000 wa jeshi la Marekani nchini Korea Kusini katika hali ambayo, jirani wa kaskazini wa nchi hiyo Korea Kaskazini imesisitiza mara kadhaa kuwa kuondoka wanajeshi hao katika Peninsula ya Korea ni moja ya masharti ya mazungumzo ya suluhu na amani kati yake na Korea Kusini.
Siku ya Ijumaa iliyopita ya tarehe 27 Aprili Rais Moon Jae-in wa Korea Kusini na mwenzake Kim Jong Un wa Korea Kaskazini walifanya mazungumzo ya kihistoria katika kijiji cha mpaka wa nchi mbili cha Panmunjom na kufikia makubaliano ya kuhakikisha silaha za nyuklia zinatokomezwa katika Peninsula ya Korea, vita vinatokomezwa kwa kufunga mkataba wa amani pamoja na kuhitimisha uhasama kati ya nchi mbili.
Marekani imekuwa ikijaribu kila mara kuonyesha na kuitangaza Korea Kaskazini kuwa ni tishio kwa eneo hilo na dunia kwa ujumla.../