Bolton: Marekani haitapunguza wanajeshi wake Korea ya Kusini
John Bolton Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani amesema kuwa Rais Donald Trump wa nchi hiyo hajaiomba Pentagon kuhusu njia mbadala zinazoweza kutekelezwa mkabala na kupunguza wanajeshi wa Marekani walioko Korea ya Kusini.
John Bolton alibainisha hayo jana baada ya gazeti la New York Times kuarifu siku ya Alhamisi kuwa Rais wa Marekani alikuwa akiangalia uwezekano wa kupunguza idadi ya wanajeshi wa nchi hiyo walioko nchini Korea ya Kusini.
Bolton amesema kuwa taarifa hiyo ya New York Times haina maana kwa kuwa Rais Trump hajaiomba Wizara ya Ulinzi (Pentagon) kuwasilisha njia mbadala ili kupunguza idadi ya wanajeshi wa Marekani walioko Korea ya Kusini. Jumatano iliyopita ofisi ya Rais wa Korea ya Kusini ilieleza kuwa kuwepo kijeshi Marekani katika nchi hiyo ya Asia kutaendelea, na hakutahusiana na makubaliano yoyote ya amani na Korea ya Kaskazini.
Huku hayo yakijiri, Seoul tayari imethibitisha pia kuwasili wiki iliyopita ndege nane za kivita aina ya F-22 za Marekani katika kituo cha kijeshi cha Korea ya Kusini katika mji wa Gwangju. Aidha ripoti zinasema kuwa maneva ya kivita kwa jina la " Max Thunder" yanatarajiwa kuanza Mei 11 mwaka huu na kudumu kwa wiki mbili ambapo karibu ndege za kivita 100 kutoka pande zote mbili zitashiriki kwenye maneva hayo.