May 09, 2018 02:57 UTC
  • Erdogan: Shakhsia wanaoiponda Qur'ani Ufaransa hawana ufahamu nayo

Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amelitaja kundi la shakhsia 300 wa Ufaransa wanaotaka kuondolewa baadhi ya aya katika kitabu kitakatifu cha Qur'ani kwa madai kuwa ni za kichochezi na zilizopitwa na wakati kuwa ni genge lisilo la maana na linalopaswa kutwezwa.

Akihutubia mkutano wa chama chake tawala jana Jumanne, Erdogan alieleza kusikitishwa kwake na kitendo hicho cha kuvunjia heshima maandiko matakatifu ya Waislamu, katika hali ambayo shakhsia hao hawana ufahamu wowote wa kitabu hicho kitukufu.

Huku akiashiria kuwa vitabu vingine vya mbinguni vimetiwa mkono na wanadamu na kuwa na mapungufu mengi, Rais wa Ututuki amesema, "Nitashangaa kama watu hao watakuwa wamesoma vitabu vyao vitukufu kama Biblia, Taurati, na Zaburi; iwapo wangelikuwa wamesoma, wangetoa wito wa kubatilishwa vitabu vyao hivyo."

Erdogan amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu akisema kuwa, "Hata kama mtashambulia kitabu chetu kitukufu, lakini sisi hatutafuata mkondo wenu huo, hatuwezi kujishusha hadhi kama nyinyi na kushambulia matukufu yenu."

Qur'ani Tukufu

Waraka uliosaniwa hivi karibuni na Makhatibu wa Sala ya Ijumaa na Maimamu zaidi ya 30 wa Ufaransa uliwataka watu wa tabaka la wasomi na wanasiasa nchini humo kutotumia ushawishi wao kuupaka matope Uislamu, wakisisitiza kuwa kitendo hicho kinaweza kuwa na matokeo mabaya ndani na nje ya nchi.

Kadhalika Katibu wa Idara Kuu ya Misri inayohusika na Fatwa za Kiislamu (Darul Iftaa), Khalid Omran alilitaja ombi hilo la raia hao 300 wa Ufaransa akiwemo Rais wa zamani wa nchi hiyo Nicolay Sarkozy na muigizaji mashuhuri Gerard Depardieu, la kutaka kufutwa baadhi ya aya au sura za Qur'ani Tukufu kuwa ni kitendo cha uchupaji mipaka na ukurasa mpya wa chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.

Tags