Waislamu wa Marekani wana hatari ya kunyanyaswa zaidi mwezi wa Ramadhani
(last modified Thu, 10 May 2018 14:31:51 GMT )
May 10, 2018 14:31 UTC
  • Waislamu wa Marekani wana hatari ya kunyanyaswa zaidi mwezi wa Ramadhani

Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu limetaka kuchukuliwa hatua za lazima za kuimarisha usalama kwa ajili ya kuwalinda Waislamu ambao wana hatari ya kukumbwa na mashambulizi na unyanyasaji zaidi katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Baraza hilo linalojulikana kwa kifupi kama CAIR ndiyo taasisi kubwa zaidi ya Waislamu wa Marekani. Limesema katika taarifa yake kwa jumuiya za Kiislamu za nchi hiyo kwamba zinapaswa kuchukua hatua za lazima za kiulinzi kwenye mwezi mtukufu wa Ramadhani hasa kwa kuzingatia kuwa idadi ya Waislamu huengezeka sana misikitini katika kipindi hicho.

Mwito huo wa Baraza la Uhusiano wa Marekani na Uislamu unaonesha namna vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji dhidi ya Waislamu vilivyo na nguvu katika kipindi cha utawala wa Donald Trump huko Marekani.

Kwa mujibu wa baraza hilo, ubaguzi, unyanyasaji na udhalilishaji unaotokana na taasubu na chuki dhidi ya Waislamu umeongezeka sana nchini Marekani tangu alipoingia madarakani rais wa nchi hiyo, Donald Trump

Polisi ya Shirikisho la Marekani FBI imetangaza kuwa, mashambulizi yanayotokana na chuki dhidi ya Waislamu yameongezeka mara tatu nchini humo tangu alipoingia madarakani Donald Trump.

Trump amekuwa akionesha chuki dhidi ya Waislamu kwa njia tofauti kama kuweka video za kuwatukana Waislamu katika ukurasa wake wa Twitter

 

Trump amekuwa akiwashambulia sana Waislamu na kuwaita eti ni magaidi na ameweka sheria za kuibana sana misikiti na maeneo ya kukusanyika Waislamu.

Hatua nyingine za kibaguzi ambazo zimeyachochea magenge yenye misimamo mikali kufanya mashambulizi dhidi ya Waislamu huko Marekani, ni sheria dhidi ya wahajiri zilizowekwa na rais huyo mwenye chuki dhidi ya wageni na hasa Waislamu bila ya kujali iwapo Waislamu hao ni raia wa Marekani au la.