Jaji wa Marekani: Yumkini Trump akauzuliwa kutokana na kesi ya ufuska
https://parstoday.ir/sw/news/world-i45480-jaji_wa_marekani_yumkini_trump_akauzuliwa_kutokana_na_kesi_ya_ufuska
Jaji mmoja nchini Marekani amesema huenda Rais Donald Trump akauzuliwa iwapo atapatikana na hatia katika kesi ya ufuska iliyowasilishwa na mwanamke mmoja ambaye anadai kudhalilishwa naye kingono.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 06, 2018 02:53 UTC
  • Jaji wa Marekani: Yumkini Trump akauzuliwa kutokana na kesi ya ufuska

Jaji mmoja nchini Marekani amesema huenda Rais Donald Trump akauzuliwa iwapo atapatikana na hatia katika kesi ya ufuska iliyowasilishwa na mwanamke mmoja ambaye anadai kudhalilishwa naye kingono.

Jaji Jennifer Schechter ameziagiza pande mbili husika katika kesi hiyo kuwasilisha ithibati zao kufikia Januari 31 mwaka ujao 2019. Mwanamke kwa jina Summer Zervos, ambaye aliwahi kuwa mshirika katika kipindi cha runinga cha "The Apprentice" kilichokuwa kikiendeshwa na Trump huko nyuma, amesema kiongozi huyo wa Marekani aliwahi kumdhalilisha kingono, kwa kumpapasa na kumbusu bila ridhaa yake.

Wakili wa mwanamke huyo, Mariann Wang amenukuliwa na jarida la Politico akisema kuwa, "Wanawake wengine waliodhalilishwa kingono na Trump wapo tayari kutoa maelezo chini ya kiapo, na tunamshangaa Trump kwa nini hataki kutoa ushahidi wake katika kesi hii iwapo hakuna kitu anachoficha."

Jaji Schechter amepuuzilia mbali hoja ya mawakili wa Trump wanaosema kuwa rais aliyeko mamlakani hawezi kushtakiwa katika mahakama ya chini, huku akisisitiza kuwa hakuna mtu ambaye yuko juu ya sheria. Hata hivyo mawakili wa Trump wamekimbia katika Mahakama Kuu ya New York kukata rufaa dhidi ya kesi hiyo.

Muigizaji wa filamu chafu za ngono Stormy Daniels aliyewahi kuwa na mahusiano na Trump

Hivi karibuni, Michael Avenatti, wakili wa muigizaji wa filamu chafu za ngono maarufu kwa jina la Stormy Daniels aliliambia gazeti la The Guardian linalochapishwa nchini Uingereza kuwa Trump atalazimika kujiuzulu baada ya kuwekwa hadharani nyaraka za sakata la kuwahi kuwa na mahusiano ya kingono na muigizaji huyo.

Mnamo mwezi Februari, sambamba na kutimia miaka miwili ya urais wa Trump, mamia ya maelfu ya wanawake waliandamana katika kila pembe ya Marekani dhidi ya kiongozi huyo.