Ban akosoa ukiukaji wa haki za binadamu duniani
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanyika kwa kisingizio cha kupambana na makundi yenye mitazamo mikali ni maafa kwa dunia ya sasa.
Ban Ki-moon amesema hayo katika ujumbe wake wa video uliotumwa kwenye Mkutano wa Amani ya Kimataifa. Amesema misimamo mikali na ya kikatili inahujumu watu, jamii na thamani za jamii ya sasa ya mwanadamu na kuongeza kuwa, jibu kwa misimamo hiyo mikali linapaswa kuheshimu sheria zinazohusiana na kulindwa kwa haki za binadamu.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, ni jambo lisilokubalika kimaadili na maafa katika mtazamo wa kistratijia kukanyagwa haki za binadamu kwa kutumia kisingizio cha kupambana na ugaidi na misimamo ya kuchupa mipaka.
Ban Ki-moon pia ameyashambulia makundi ya kigaidi ambayo amesema yamekuwa yakilenga raia wasio na hatia na kuhujumu maadili na thamani za kibinadamu.