Marekani kujiondoa kwenye Baraza la Haki za Binadamu la UN
https://parstoday.ir/sw/news/world-i45924-marekani_kujiondoa_kwenye_baraza_la_haki_za_binadamu_la_un
Duru za kidiplomasia zimedokeza kuwa, yumkini Marekani ikajiondoa kwenye Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ndani ya siku chache zijazo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 16, 2018 03:07 UTC
  • Marekani kujiondoa kwenye Baraza la Haki za Binadamu la UN

Duru za kidiplomasia zimedokeza kuwa, yumkini Marekani ikajiondoa kwenye Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ndani ya siku chache zijazo.

Mwanadiplomasia wa Marekani na mwingine wa mojawapo ya nchi za Magharibi ambao hawakutana majina yao yatajwe wameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, rais wa Marekani anatazamiwa kutoa tangazo hilo la kuiondoa nchi hiyo katika baraza hilo kufikia Jumanne ijayo, ikiwa ni katika mfululizo wa hatua za Donald Trump za kuiondoa Marekani katika taasisi muhimu za kimataifa.

Tayari Marekani imeshajiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya Iran ya JCPOA, Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Paris na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO.

Trump baada ya kuiondoa Marekani kwenye makubaliano ya JCPOA

Mwaka jana, Nikki Haley, Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa alidokeza juu ya uwezekano wa kujiondoa Washington kwenye Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kwa lengo la kuukingia kifua utawala haramu wa Israel. Alidai kuwa, Washington inataka mabadiliko yafanyike katika baraza hilo na kufutwa sera eti zilizo dhidi ya Israel.

Baraza hilo limepasisha maazimio zaidi ya 70 ya kulaani ukiukaji wa haki za binadamu wa Israel dhidi ya Wapalestina.

Marekani ambayo imekuwa ikidai kuwa ni miongoni mwa nchi zenye mfumo wa demokrasia na mtetezi wa haki za binadamu duniani,  imekuwa kimya kuhusu jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina ambao ardhi zao zinakaliwa kwa mabavu; sambamba na kufumbia macho ukiukaji wa haki za binadamu nchini Saudi Arabia na hata mauaji ya raia wa Yemen yanayofanywa na utawala wa Aal-Saud.