Trump afuta ratiba ya maneva ya kijeshi na Korea Kusini
Rais Donald Trump wa Marekani amefuta ratiba ya maneva ya kijeshi yaliyokuwa yamepangwa kufanyika kati ya jeshi la Marekani na Korea Kusini kutokana na gharama.
Afisa mmoja wa Marekani ambaye hakutaka kutaja jina lake amesema kuwa, baada ya kubainika kiwango kikubwa cha gharama ya maneva hayo ya pamoja ya kijeshi kati ya jeshi la Marekani na Korea Kusini, Rais Trump ameamua kuyafuta. Kwa mujibu wa afisa huyo wa Marekani, gharama ya maneva hayo ni karibu Dola milioni 14. Mwezi uliopita Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) ilisimamisha maneva ya kijeshi yaliyopewa jina la 'Freedom Guardian' ikiwa ni katika juhudi za kuunga mkono kikao cha Rais Donald Trump na Kim Jong-un wa Korea Kaskazini nchini Singapore. Mwaka jana jumla ya askari elfu 17 na 500 wa Marekani na wengine zaidi ya elfu 50 wa Korea Kusini, walishiriki maneva hayo ya kijeshi ya Freedom Guardian.
Aidha maneva hayo yaliwashirikisha askari wa Australia, Canada, Colombia, Denmark, New Zealand, Uholanzi na Uingereza. Mara zote viongozi wa Marekani wamekuwa wakidai kuwa maneva ya kijeshi inayoyafanya kwa kushirikiana na washirika wake, ni kwa ajili ya kuliweka tayari jeshi la nchi hiyo na pia kuvutia uaminifu kwa marafiki wake. Hata hivyo hatua ya sasa ya Trump ya kufuta ratiba ya maneva ya sasa imewashangaza sana washirika wake na hata viongozi wa ngazi za juu nchini Marekani.