Wasiwasi wa Marekani juu ya kupanuka zaidi harakati ya kususiwa Israel
Balozi na mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Nikki Haley amehutubia mkutano wa jumuiya ya Muungano wa Wakristo kwa Ajili ya Israel (Christians United for Israel) ambako ametoa wito wa kukabiliana na harakati ya kususiwa utawala wa Kizayuni wa Israel, BDS kwa kifupi.
Haley amekiri kwamba mwenendo wa kuipinga Israel unaongezeka hata ndani ya Marekani na kwamba baadhi ya nchi zinatangaza waziwazi kwamba zinataka kuangamizwa kabisa utawala huo.
Kupanuka zaidi harakati ya kimataifa ya kususiwa utawala haramu wa Israel na taathira zake kwa utawala huo vimeilazimisha Marekani kuingilia kati, suala ambalo linaonesha kuwa, harakati hiyo inafanikiwa kwa kadiri kwamba, viongozi wa ngazi za juu wa serikali ya Washington wanalazimika kufanya jitihada za kupunguza mashinikizo yanayoulemea utawala ghasibu wa Israel kutokana na harakati hiyo. Kwa hakika kupanuka zaidi harakati ya BDS inayotoa wito wa kususiwa Israel katika masuala mbalimbali na kujiunga makundi mengi ya Wayahudi duniani na harakati hiyo ni kielelezo cha walimwengu kuonesha mshikamano wao na watu wanaodhulumiwa wa Palestina. Makundi ya Kiyahudi katika maeneo mbalimbali ya dunia yametangaza kuwa, kujiunga na harakati hiyo hakuna maana ya kupiga vita Uyahudi bali ni kuwatetea Wapalestina wanaopigania haki na uadilifu.
Harakati ya kususiwa Israel ya Boycott, Divestment and Sanctions (BDS) imeshika kasi sana katika nchi za Ulaya, Marekani na nchi za America ya Latini hususan katika vyuo vikuu. Wasiwasi mkubwa wa Wazayuni ni kwamba harakati hiyo inashamiri zaidi kati ya wanafunzi wa vyuo vikuu na wahadhiri wao ambao wanatambuliwa kuwa wasomi wa kila jamii, na suala hilo ni pigo lisiloweza kufidiwa kwa Wazayuni maghasibu.
Siku chache zilizopita pia Baraza Kuu la Usoshalisti wa Kimataifa lenye nchi wanachama zaidi ya 140 lilikutana katika makao ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva na kupasisha hati ya kususiwa Israel, kuondoa rasilimali zao katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo na kuiwekea vikwazo Israel.
Harakati hiyo imeanzisha mashirika katika nchi kama Australia, Canada, Marekani, Ufaransa, Uingereza, Jordan na Afrika Kusini yanayotaka kususiwa Israel katika nyanja tatu muhimu za uchumi, utamaduni na masuala ya kielimu. Malengo mengine ya harakati hiyo ni kuangamiza nguvu na uwezo wa Israel, kukomesha uvamizi na ukoloni wa utawala huo ghasibu katika ardhi inayokaliwa kwa mabavu ya Palestina na kutambuliwa rasmi haki za kimsingi za raia wa Palestina.
Kukua na kupanuka kila uchao shughuli za harakati hiyo katika maeneno mbalimbali duniani hususan katika nchi za Magharibi kunazidisha wahka na wasiwasi wa viongozi wa utawala haramu wa Israel na na mtetezi wake mkuu yaani Marekani. Matangazo ya harakati hiyo ambayo yanarushwa hewani na vyombo vya habari vikiwemo vya baadhi ya nchi za Magharibi yamezidisha wasiwasi huo.
Kuhusu suala hilo Pofesa Ellan Dirshowitz ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Harvard anasema harakati ya kimataifa ya kususiwa Israel BSD ni tishio la kistratijia kwa utawala huo wa Kizayuni katika siku za usoni na inaweka alama ya kuuliza kuhusu uhalali wa kuwepo dola la Israel.
Kwa ujumla ni kwamba harakati ya kususiwa Israel inaendelea kupanuka siku baada ya siku katika maeneo mbalimbali dunia na kutoa wito wa kutengwa utawala huo haramu licha ya lobi na makundi yya mashinikizo Wazayuni hususan katika nchi za Magharibi.