Mkutano wa viongozi wa BRICS na ukosoaji wa sera za Marekani
Sera za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja za Marekani ambazo zimeshika kasi zaidi katika utawala wa Donald Trump zimekuwa kero kwa aghlabu ya mataifa yote huru na yanayojitawala duniani.
China na Russia ambazo ni madola mawili makubwa yaliyolengwa zaidi kwa siasa za kihasama za Marekani daima zimekuwa zikikosoa sera hizo za serikali ya Washington. Mkutano wa 10 wa BRICS ulioanza Jumatano iliyopita mjini Johannesburg huko Afrika Kusini ni fursa nzuri ya kukosoa sera za Marekani za kujichukulia maamuzi ya upande mmoja kuhusu masuala ya kimataifa. Mkutano huo unaozishirikisha nchi wanachama yaani Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini unamaliza kazi zake leo tarehe 27 Julai.
Rais Xi Jinping wa China amesema katika hotuba yake kwenye mkutano huo kwamba; Sera za kujichukulia maamuzi na misimamo ya upande mmoja zinazidi kuongezeka na zinatoa pigo kwa mfumo wa biashara inayoshirikisha mataifa kadhaa. Jinping ambaye nchi yake imeingia katika vita vya kibiashara na Marekani baada ya Rais wa nchi hiyo Donald Trump kuzidisha ushuru wa forodha wa bidhaa kutoka China, amesema kuwa, nchi zinazotaka kudhibiti uchumi wa dunia hatimaye zitapata madhara na kugonga mwamba.
Ukosoaji mkali wa Rais wa China unafanana na sana na misimamo ya Rais Vladimir Putin wa Russia ambayo ni miongoni mwa nchi wanachama wa kundi la BRICS. Marais wa China na Russia wanaamini kuwa, hali ya kimataifa na mfumo wa sasa unaielekeza dunia katika mfumo wa kambi kadhaa lakini Marekani inafuatilia malengo yake kwa kudumisha sera za kujichukua maamuzi na misimamo ya upande mmoja na kutaka kuwa polisi wa dunia.
Sera na siasa hizo za Marekani za kutaka kuwa nguvu pekee katika mfumo inaoutaka yenyewe wa kambi moja pia zimekuwa zikikosolewa vikali na Rais Vladimir Putin wa Russia. Putin anaamini kuwa, sera hizo za Marekani zinakwamisha na kukwaza kazi za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusababisha machafuko na migogoro katika uga wa kimataifa. Putin anasema: "Mfumo wa kambi moja chini ya uongozi wa Marekani kamwe hauwezi kukubaliwa na Russia."
Moscow inaamini kuwa, ushirikiano mwema wa Russia na China unaweza kuwa kigezo cha kuigwa na nchi mbalimbali katika karne hii ya 21. Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia anatoa mfano wa ushirikiano huo mzuri kwa kuashiria ushirikiano wa pande hizo mbili katika jumuiya kama BRICS, The Shanghai Cooperation Organisation (SCO), Eurasian Economic Union na kadhalika. China na Russia pia zinaamini kwamba, kutokana na mabadiliko yaliyotokea katika nyanja za kiuchumi na kisiasa, makundi na jumuiya mpya za kimataifa zinapaswa kuchukua nafasi ya jumuiya za zamani ambazo zimepoteza taathira zao baada ya kutoweka sababu na falsafa zilizopelekea kuanzishwa kwao. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana nchi hizo mbili zikazidisha mikakati ya kuhakikisha makundi na jumuiya kama BRICS na G20 zinakuwa na nguvu na taathira kubwa zaidi.
Katika upande mwingine Marekani inapinga vikali mwelekeo huo na inafanya jitihada za kuhakikisha kwamba inakuwa nguvu kubwa na ya kipekee katika uwanja wa kimataifa. Hata hivyo ushahidi unaonesha kuwa, sera hizo za Marekani zinaifanya nchi hiyo itengwe zaidi siku baada ya siku katika medani ya kimataifa.