Seneta Sanders akosoa vikali mfumo wa sheria wa mahakama za Marekani
Seneta Bernie Sanders wa jimbo la Vermont amesema mfumo wa sheria wa mahakama za Marekani ni wa kionevu na upendeleo.
Sanders ameyasema hayo katika andiko la ukumbusho kwa vyombo vya habari na kueleza kwamba, kuna malaki ya watu ambao wamewekwa jela ilhali bado haijathibitishwa kama wamefanya makosa ya uhalifu.
Kwa mujibu wa Seneta huyo, zaidi ya asilimia 65 ya watu waliofungwa jela mwaka 2016 nchini Marekani hawakushtakiwa na kuhukumiwa mahakamani; ikimaanisha kwamba zaidi ya watu laki nne walifungwa jela bila ya kushtakiwa kwa makosa waliyofanya au bila hata kufanya kosa lolote.
Seneta Bernie Sanders ameongeza kuwa watu hao waliwekwa jela kwa sababu tu hawakuwa na pesa za kutoa kwa ajili ya kupewa dhamana.
Sanders ametaka ufanyiwe marekebisho ule aliouita "mfumo wenye kasoro" ambao amesema unawaadhibu Wamarekani kwa makosa ya uhalifu ambayo hawajafanya.
Ukosoaji huo unafanywa katika hali ambayo kwa mujibu wa takwimu, mfumo wa sheria wa mahakama za Marekani una ubaguzi mkubwa dhidi ya raia wa nchi hiyo wasio wazungu na wale wenye asili ya Afrika.../