Daily Mail: MOSSAD inaongoza kwa mauaji ya kigaidi duniani
Gazeti la Daily Mail la Uingereza limeripoti kuwa shirika la ujasusi la Israel Mossad linaongoza duniani kwa kufanya mauaji ya kigaidi.
Ripoti iliyochapishwa na gazeti hilo la Uingereza imesema kuwa, katika kipindi cha miaka 10 tu iliyopita Mossad imefanya operesheni 800 za mauaji ya kigaidi ambazo zimepelekea kuuawa maelfu ya watu.
Ripoti hiyo imesema kuwa, maajenti wa Mossad wameuwa watu wengi zaidi kuliko shirika la ujasusi la nchi yoyote ile duniani baada ya Vita vya Pili vya Dunia.
Gazeti la Daily Mail limeandika kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel sasa limekuwa kinara wa mauaji ya kigaidi duniani na kwamba idadi ya mauaji ya shirika hilo haina kifani. Limeongeza kuwa, Mossad si tu kwamba, imefanya mauaji mengi zaidi ya kigaidi baada ya Vita vya Pili vya Dunia bali pia imezidisha kasi ya mauaji.
Gazeti hilo limeashiria operesheni ya kigaidi iliyofanywa na Mossad tarehe 10 Januari mwaka 1978 na kusema kuwa, maajenti wa Mossad walifanya mauaji ya kigaidi dhidi ya Palestina kwa kutumia dawa ya mswaki iliyojazwa sumu hatari.