Korea Kaskazini yapinga mpango wa Japan wa kuweka ngao ya makombora
Serikali ya Korea Kaskazini im imekosoa hatua ya Japan ya kutaka kuweka ngao ya makombora ndani ya nchi hiyo na kuongeza kuwa Shinzō Abe, Waziri Mkuu wa Japan anakusudia kuibadili nchi yake iwe dola lenye nguvu za kijeshi.
Taarifa iliyotolewa na gazeti la Rodong Sinmun la Korea Kaskazini imesema kuwa, katika hali ambayo serikali ya Pyongyang inafanya juhudi za kutokomeza kikamilifu makombora yake, nchi jirani (Japan) inajizatiti kwa mfumo wa makombora. Aidha gazeti hilo limeongeza kwamba hatua hiyo ya Japan ya kusimika ngao hiyo ya makombora katika pwani ya nchi hiyo, ni mbinu na hila za Tokyo za kupunguza wasi wasi unaoongezeka na upinzani wa raia wa nchi hiyo, na haina njia yoyote ya kuihalalisha.

Kadhalika gazeti la Rodong Sinmun limeituhumu serikali ya Tokyo kuwa inafanya njama za kutibua mwenendo wa maridhiano na kupunguza mzozo ndani ya eneo la Korea, na kuhusiana na hilo limewataka viongozi wa Japan kuachana na mpango hatari wa kuibadili nchi hiyo kuwa dola lenye nguvu za kijeshi na badala yake kufuata mwenendo wenye lengo la kuimarisha usalama katika eneo. Serikali ya Japan na katika kujizatiti kwa mfumo wa kiulinzi na kukabiliana na vitisho vya makombora na silaha za nyuklia za Korea Kaskazini, inakusudia kusimika mfumo wa kukabiliana na makombora katika miji ya Akita na Yamaguchi, hatua ambayo imeibua hali ya wasi wasi mkubwa kwa wakazi walioko jirani na maeneo hayo.