Putin: Operesheni za anga za Israel zinakiuka uhuru wa kujitawala Syria
Rais Vladimir Putin wa Russia amesema operesheni za anga za jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika anga ya Syria ni ukiukaji wa mamlaka na kujitawala serikali halali ya sasa ya Damascus. Putin amesema hayo huku mgogoro kuhusu ajali ya kutunguliwa ndege ya Russia katika anga ya Syria wakati wa shambulio la utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya nchi hiyo Kiarabu ukiendelea kutokota.
Ikulu ya Russia (Kremlin) imemnukuu Putin akiyasema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Putin amesisitiza kuwa, Tel Aviv inafanya mashambulizi ya anga nchini Syria bila idhini na ridhaa ya serikali ya Damascus. Ingawaje Putin hajaulumu moja kwa moja utawala huo pandikizi kuhusu kutunguliwa kwa ndege ya kijeshi ya Russia, lakini hapo jana Waziri wa Ulinzi wa Russia Sergueï Choïgou alitoa onyo kwa Waziri wa Vita wa utawala wa Kizayuni Avigdor Lieberman na kumweleza kwamba Moscow inaibebesha Tel Aviv dhima kamili ya vifo vya wanajeshi wake 15 katika ajali hiyo.

Jana Jumanne, Wizara ya Ulinzi ya Russia ilitangaza kuwa ndege moja ya kijeshi aina ya Ilyushin 20 (IL20) ikiwa na watu 15 ndani yake ilipotea kwenye rada karibu na kituo cha anga cha Hamimim mkoani Lattakia kaskazini magharibi mwa Syria.
Marekani na nchi kadhaa waitifaki wake ziliunda muungano eti dhidi kundi la kigaidi la Daesh tangu Agosti mwaka 2014 nje ya fremu ya Umoja wa Mataifa na pasina na kuwasiliana na serikali ya Syria. Muungano huo vamizi unaoongozwa na Marekani hadi sasa umeuwa raia wengi wasio na hatia.