Nov 13, 2018 13:13 UTC
  • Misimamo inayogongana ya Trump mkabala na mamlaka ya kiulinzi ya Ulaya

Hitilafu na mizozo baina ya Ulaya na Marekani imedhihiri hivi sasa kuliko kipindi kingine chochote kile tangu Rais Donald Trump wa Marekani aingie madarakani.

Hitilafu hizo ambazo zimechukua wigo mpana zaidi zinajumuisha masuala kama ya mkataba wa tabianchi wa Paris Ufaransa, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, biashara na vilevile mchango wa Ulaya katika Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) na mamlaka ya kiulinzi ya Ulaya. Suala hilo hususan baada ya msimamo uliozua makelele mengi wa Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kuhusiana na udharura wa Ulaya kuwa na mamlaka na kujitegemea kiulinzi na kuanzishwa jeshi la Ulaya limekuwa changamoto kubwa kwa pande mbili.

Mwanzoni mwa safari yake hivi karibuni huko Paris Ufaransa kwa ajili ya kushiriki katika kumbukumbu ya miaka 100 tangu kumalizika Vita Vikuu ya Kwanza ya Dunia, Trump alikosoa vikali matamshi ya Rais Macron kuhusu udharura wa kuundwa jeshi la Ulaya na kuyataja kuwa ni ya dharau na ya uvunjiaji wa heshima. Trump alisisitiza katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Pendekezo la Macron la Ulaya kuwa la kikosi chake maalumu cha jeshi kwa ajili ya kujilinda mkabala na Marekani, Russia na China ni matamshi ya uvunjiaji heshima.

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa

Pamoja na hayo, Rais Macron hata baada ya kukutana na Donald Trump kwa mara nyingine tena alisisitiza msimamo wake wa hapo kabla ambapo alikwenda mbali zaidi na kukosoa vikali hatua ya baadhi ya nchi za Ulaya ya kununua silaha za Marekani. Kwa hakika msimamo huo ulikuwa pigo kubwa kwa Trump ambaye licha ya kukutana ana kwa ana na Macron lakini alishindwa kumshawishi kiongozi huyo wa Ufaransa abadilishe msimamo wake. Baada ya Trump kurejea nchini Marekani hapo jana Jumatatu, kwa mara nyingine tena alizungumzia suala la Marekani kubeba mzigo wa ulinzi wa Ulaya na kutaka madola ya Ulaya yalipe michango yao na ghara ya mzigo huo. 

Katika ujumbe wake huo wa Twitter, Trump  hakuzihutubu nchi za Ulaya tu, bali aliwaambia pia washirika wengine wa Marekani na nchi nyingine ulimwenguni na kusisitiza ulazima wa kulipa gharama za ulinzi zinaopatiwa na Marekani. Trump alidai kwamba: Fedha nyingi zinatumika kwa ajili ya kutoa ulinzi kwa nchi nyingine na nchi hizi ambazo ni tajiri sana zinapaswa kuilipa Marekani gharama za ulinzi vinginevyo zijilinde zenyewe.

Kimsingi ni kuwa, Trump alikuwa akiwahutubu washirika wa Marekani katika maeneo mbalimbali ya dunia kuanzia Saudi Arabia, Japan hadi Korea Kusini na Ulaya. Wakati huo huo, msimamo huu wa Trump una ishara za kukinzana  waziwazi na utendaji wa kiusalama na kijeshi wa kiongozi huyo wa Marekani. Kwa upande mmoja Trump anapinga vikali hatua yoyote ile ya Ulaya ya kutaka kujitegemea kiulinzi na kutokuwa tegemezi kwa Washington katika uwanja huo, na kwa upande wa pili anawatawaka washirika wa Marekani hususan Ulaya walipe gharama za kupatiwa ulinzi na usalama na Washington!

Rais Donald Trump akiwa na mfalme Salman bin Abdul Aziz wa Saudi Arabia moja ya washirika wakuu wa Marekani

Ukweli wa mambo ni kuwa, daima Marekani imekuwa ikitaka Ulaya iwe tegemezi kwake katika mambo mbalimbali ukiwemo uwanja wa kijeshi na kiusalama, ili kwa utaratibu huo si tu kwamba, ipate wasaa wa kuendelea kuweko kijeshi huko Ulaya, bali kupitia njia hiyo iweze kupenyeza siasa zake za kiulinzi na za kigeni katika nchi za bara hilo.

Donald Tusk Mkuu wa Baraza la Ulaya anasema: Kwa mara ya kwanza katika historia, tumeshuhudia nchini Marekani kuweko serikali ambayo haitaki kuona kunakuweko Ulaya yenye umoja na nguvu. Pamoja na hayo, hali hii si yenye kuvumilika tena barani Ulaya hasa kwa nchi muhimu na zenye taathira katika Umoja wa Ulaya yaani Ufaransa na Ujerumani na ndio maana zinataka kuweko mageuzi katika masuala ya usalama na ulinzi na kuelekea upande wa kiigizo cha mhimili wa Ulaya.

Rais Macron anataka kushirikishwa katika muundo mpya wa usalama wa Ulaya hata nchi kama Russia. Jambo hilo limezidisha maradufu hasira za Marekani, hasa kwa kutilia maanani kwamba, kwa miaka kadhaa sasa Washington imekuwa ikifanya juhudi za kuidhihirisha Russia kuwa ndiye adui mkuu wa Magharibi na Ulaya. Licha ya upinzani wa Marekani, lakini madola ya Ulaya yamepiga hatua kubwa katika njia ya kuanzisha muundo huru na unaojitegemea wa kiulinzi, hatua ambayo itakuwa na maana ya kupungua taathira na ushawishi wa Marekani.

Tags