Nov 14, 2018 02:39 UTC
  • UN: Waislamu wa Rohingya wanakabiliwa na hatari kubwa wakirejeshwa Myanmar

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameitaka serikali ya Bangladesh kusimamisha mpango wake wa kuwarejesha kwa nguvu nchini Myanmar maelfu ya wakimbizi Waislamu wa Rohingya akisisitiza kuwa maisha yao yatakuwa hatarini.

Michelle Bachelet alitoa mwito huo jana Jumanne na kuongeza kuwa, mbali na kuyaweka hatarini maisha ya wakimbizi wa Warohingya wanaotafuta hifadhi nchini Bangladesh, kuwarejesha pia kwa nguvu wakimbizi hao nchini kwao ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa.

Amesema Bangladesh inapaswa kuangalia upya uamuzi wake wa kuwarejesha kwa nguvu wakimbizi 2,200 wa Kirohingya nchini Myanmar kwani mazingira ya kuwapokea hayajaandaliwa.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet 

Amesema, "kuna hali ya taharuki katika kambi za wakimbizi za Cox’s Bazar. Tumepokea habari ya kujaribu kujitoa uhai wakimbizi wawili wa Rohingya wakihofia kurejeshwa nchini Myanmar."

Kwa mujibu wa UN, zaidi ya wakimbizi Waislamu wa Rohingya 700,000 wamekimbilia nchini Bangladesh tangu Agosti mwaka jana 2017, baada ya wanajeshi wa Myanmar wakishirikiana na Mabudha wenye misimamo mikali kuanzisha wimbi jipya la mauaji na hujuma dhidi ya Warohingya katika mkoa wa Rakhine nchini Myanmar.  

Ripoti hiyo iliyotolewa hivi karibuni na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR na Mpango wa Ujenzi wa umoja huo ilisisitiza kuwa Waislamu Warohingya wangali wanaishi kwa hofu na kutokuwa na imani yoyote kuhusu usalama wao wakiwa hawana hata ruhusa ya kutembea kwa uhuru katika eneo wanaloishi la mkoa wa Rakhine. 

Mwezi uliopita, wakimbizi Waislamu wa jamii ya Rohingya wanaoishi kambini nchini India walisema afadhali wauawe wakiwa ndani ya nchi hiyo badala ya kurejeshwa nchini kwao Myanmar.

Tags