May 15, 2019 03:41 UTC
  • WHO: Watu Milioni 50 wanaugua ugonjwa wa kusahau duniani

Shirika la Afya Duniani WHO limesema watu takriban milioni 50 kote ulimwenguni wanaugua ugonjwa wa kusahau (Dementia) huku idadi hii ikitabiriwa kuongezeka mara tatu ifikapo mwaka 2050.

WHO imetoa taarifa hiyo sambamba na kutoa mwongozo mpya wa kusaidia watu kupunguza hatari za ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu au kusahau. Muongozo huo pamoja na mambo mengine unataja masuala kama vile kufanya mazoezi mara kwa mara, kutovuta sigara, kuepuka matumizi hatari ya pombe  na kudumisha lishe bora kama mojawapo ya njia za kuboresha afya ya wanadamu na kuwasaidia kuepuka hatari ya ugonjwa huo.

Akizungumza katika uzinduzi wa mwongozo huo mjini Geneva Uswisi jana Jumanne  Dkt. Neerja Chowdhury, Mkurugenzi mkuu katika kitengo cha afya ya akili na matumizi ya mihadarati, WHO amesema kwa sasa kuna wagonjwa takriban milioni 50 wa kupoteza kumbukumbu kote ulimwenguni idadi hii ikitarajiwa kuongezeka mara tatu ifikapo mwaka 2050

Amesema ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu sio tu unaathiri mgonjwa lakini pia familia yake, walezi na una gharama za kiuchumi kwa jamii, ikitarajiwa kwamba ifikapo mwaka 2030 gharama hiyo itafikia dola trilioni 2 kila mwaka.

Matibau ya ugonjwa wa kusahau (Dementia)

WHO inasema kwamba watu walio na ugonjwa huo wanakabiliwa na hatari ya kunyanyapaliwa kutokana na ukosefu wa taarifa na kwa kuwa hakuna tiba kwa sasa, WHO inasisitiza umuhimu wa kuzuia ambapo muongozo huo unalenga kushughulikia suala hilo.

Ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu unasababisha mtu kupoteza uwezo wa kuelewa, unaathiri kumbukumbu, mawazo, uwezo wa kujifunza, lugha na unatokana na baadhi ya magonjwa au majeraha ambayo yanaathiri ubongo.

 

Tags