China yaituhumu Marekani kuwa inatekeleza 'Ugaidi wa Kiuchumi'
China imeituhumu Marekani kuwa inachochea kwa makusudi mizozo ya kibiashara ambayo ni sawa na 'ugaidi wa wazi wa kiuchumi.'
Akizungumza Alhamisi mjini Beijing, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa China Zhang Hanhui amesema, "Tunapinga vita vya kibiashara, lakini hatuviogopi."
Ameendelea kusema kuwa: "Kuchochea mgogoro wa kibiashara kwa makusudi ni ugaidi wa wazi wa kiuchumi na pia ni ubabe wa kiuchumi." Amesema China inapinga hatua ya Marekani kutumia sera za vikwazo, kuongeza ushuru wa forodha na kulinda viwanda vya ndani.
Waziri huyo wa China ametahadharisha kuwa hakutakuwa na mshindi katika vita vya kibiashara na kuongeza kuwa vita hivyo vitakuwa na taathira hasi kwa ustawi na uhuishaji wa uchumi wa dunia.
Mgogoro wa kiuchumi wa China na Marekani umezidi kuwa mbaya baada ya Rais Trump kuongeza ushuru wa forodha kwa bidhaa za China huku akiliwekea vikwazo shirika la mawasiliano la China, Huawei.

Hivi karibuni Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China alisema kuwa, Marekani inazuia kufanyika mazungumzo ya kibiashara ya pande mbili.
Lu Kang sambamba na kufafanua kuwa, msimamo wa Beijing unaweka wazi kwamba, tofauti zilizopo za kibiashara kati yake na Marekani zinawezekana kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo.
Aidha Wizara ya Biashara ya China imetoa taarifa ambapo sanjari na kupinga vikwazo vya upande mmoja vya Marekani dhidi ya nchi nyingine, imeitaka Washington kusimamisha hatua zake hizo mbovu.