Donald Trump akaribishwa kwa maandamano mjini London Uingereza
https://parstoday.ir/sw/news/world-i53896-donald_trump_akaribishwa_kwa_maandamano_mjini_london_uingereza
Rais Donald Trump wa Marekani amewasili katika mji mkuu wa Uingereza huku kukiwa na maandamano makubwa ya wananchi wenye hasira wanaompinga kiongozi huyo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jun 03, 2019 08:12 UTC
  • Donald Trump akaribishwa kwa maandamano mjini London Uingereza

Rais Donald Trump wa Marekani amewasili katika mji mkuu wa Uingereza huku kukiwa na maandamano makubwa ya wananchi wenye hasira wanaompinga kiongozi huyo.

Trump akiwa ameandamana na mke wake, Melania, waliwasili London leo Jumatatu asubuhi kwa safari ya siku tatu ambapo anatazamiwa kukutana na Malikia Elizabeth wa Pili na waziri mkuu anayeondoka Theresa May.

Mamia ya maelfu ya raia wa Uingereza wameapa kukwamisha shughuli zote za mji wa London wakati wa safari ya Trump mjini huo. Safari hiyo ya Trump pia imekosolewa na wanasiasa wa ngazi za juu wa Uingereza ambao wamesema mtawala huyo wa Marekani hastahiki kualikwa na Malkia kutembelea nchi hiyo.

Trump pia ameingilia mambo ya ndani ya Uingereza kwa kutangaza kuwa, anamuunga mkono Boris Johnson kuwa waiziri mkuu wa nchi hiyo baada ya Theresa May kutangaza kujiuzulu.

Kiongozi wa chama cha upinzani cha Leba, Jeremy Corbyn amemkosoa vikali Trump na kusema matamshi yake ni uingiliaji usiokubalika wa demokrasia ya Uingereza.

Maandamano dhidi ya Trump mjini London

Trump pia amerushiana maneneo makali na Meya wa London, Sadiq Khan. Katika makala aliyoandika kwenye gazeti la Guardian, Khan amemfananisha Trump na wafashisti wa karne ya 20 barani Ulaya. Amesema katika miaka ijayo, safari ya Trump nchini Uingereza itatazamwa kwa masikitiko makubwa.

Trump naye amemjibu Khan na kumtaja kuwa Meya aliyefeli katika kazi zake na asiyefaa.

Safari ya Trump mjini London imeshushwa hadhi kwani hatakagua gwaride maalumu wala hatazungushwa London kwa farasi kama ilivyo kwa marais wanaopewa heshima na taadhima wala hataruhusiwa kuhutubia Bunge la Uingereza.