China yaitaka Marekani isitishe mashinikizo yake dhidi ya Iran
China imeionya vikali Marekani kuhusu taathira hasi ya kutangaza kuwa itatuma wanajeshi 1,000 wa ziada katika eneo la Asia Magharibi (Mashariki ya Kati); huku ikiitaka Washington ikomeshe mashinikizo yake ya kuchupa mipaka dhidi ya Tehran.
Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi pia amesema mashinikizo hayo ya kuchupa mipaka dhidi ya Iran yanaweza kusababisha maafa makubwa katika eneo.
Wanga Yi alisema hayo jana mjini Beijing katika mkutano wake na mwenzake wa Syria, Walid Muallem, ambapo pia ameisihi Iran isijitenga na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kiwepesi, licha ya mashinikizo dhidi yake.
Ameeleza bayana kuwa, "Katika hali ya hivi sasa, tunatarajia kuwa Iran itafanya maamuzi ya busara ya kutoachana na makubaliano ya nyuklia kwa urahisi. Wakati huo huo tunatarajia pande nyingine zitaheshimu haki na maslahi ya upande wa Iran na kuchukua hatua za kweli za kuilinda mapatano ya JCPOA."
Siku ya Jumatatu, Marekani ilitangaza kuwa itatuma wanajeshi elfu moja zaidi katika eneo la Asia Magharibi pamoja na kutoa picha kadhaa ambazo inasema ni ushahidi mwingine kwamba Iran ilihusika na mashambulizi dhidi ya meli za kubeba mafuta yaliyotokea katika Bahari ya Oman wiki iliyopita. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha vikali madai hayo yasiyo na msingi.
Aidha hivi karibuni serikali ya Marekani na katika kuendeleza siasa zake za uhasama dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ilituma meli kadhaa zenye silaha na meli inayobeba ndege za kivita katika eneo la Ghuba ya Uajemi.