Maduro: Jaribio lililofeli la kutaka kuniua liligharimu dola milioni 20
Rais wa Venezuela amemtuhumu mbunge mmoja wa upinzani kwa kuiba kitita kikubwa cha fedha ili kutekeleza njama ya mauaji dhidi yake mwezi Agosti mwaka jana.
Rais Nicolaus Maduro wa Venezuela alisema jana katika hafla ya kijeshi huko Caracas mji mkuu wa nchi hiyo kuwa na hapa ninamnukuu, "leo tunafahamu vyema namna mpango huo wa kutaka kuniua ulivyoratibiwa huko Colombia na ni mtu gani aliyetoa fedha hizo." Mwisho wa kunukuu. Maduro ameongeza kuwa njama hiyo ya kutaka kumuua iligharimu mamilioni ya dola, na kwamba kiasi hicho kilikuwa cha dola milioni 20.
Rais wa Venezuela amebainisha kuwa fedha hizo ziliporwa na Julio Borges shakhsia wa upinzani nchini humo. Mwezi Agosti mwaka jana ndege isiyo na rubani (droni) iliyokuwa imebeba mada za milipuko ilifika hadi mahali ambapo Rais Maduro alikuwa akihutubia kwa lengo la kumuua, hata hivyo jaribio hilo liligonga mwamba. Mlinzi mmoja wa Rais Maduro alijeruhiwa na kisha ndege hiyo isiyo na rubani ikalipuka baada ya kugonga nyumba. Tukio hili tajwa lilitokea wakati televisheni ya taifa ya Venezuela ilikuwa ikitangaza moja kwa moja hotuba iliyokuwa ikitolewa na Rais Maduro mbele ya hadhara ya wanajeshi katika mji mkuu, Caracas. Rais wa Venezuela alilazimika kukatisha hotuba yake na kuondoka hapo baada ya tukio hilo. Rais Nicolaus Maduro hakupata madhara yoyote lakini askari saba wa kikosi cha gadi ya taifa walijeruhiwa.
Miezi kadhaa iliyopita Venezuela ilikumbwa na mgogoro kutokana na uingiliaji wa Marekani na uungaji mkono wake kwa wapinzani wa serikali ya Caracas.